Sheria mpya kudhibiti uhamiaji Ujerumani
3 Februari 2016Muswada wa sheria hiyo unahusisha pia kuanzishwa kwa vituo maalumu vya mapokezi kwenye mipaka ambako maombi ya wahamiaji wanaotafuta hifadhi kutoka mataifa yanayochukuliwa kusa salaama yanasguhulikiwa haraka na yumkini kurejeshwa makwao.
Hatua zilizotajwa katika pendekezo la muswada huo zitasitisha kuungana kwa familia kwa muda wa miaka miwili, kwa wahamiaji ambao hawapati hadhi ya moja kwa moja ya ukimbizi chini ya mikataba ya kimataifa, lakini ambao wanaweza kukabiliwa na mateso iwapo watarudishwa nyumbani kwao.
Sheria hizo ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa na Merkel kuimarisha taratibu za maombi ya hifadhi nchini Ujerumani, kuelekea uchaguzi muhimu wa majimbo mwezi ujao.
AfD yatumia mgogoro kujiimarisha
Kura za maoni zinaonyesha kuwa chama kinachopinga uhamiaji cha Alternative für Deutschland - au Chama Mbadala cha Ujerumani, huenda kikafanya vizuri katika majimbo ya Baden Würtenberg, Rheinland-Palatinate na Saxony Anhalt.
Uungwaji mkono wa chama cha Merkel cha Christian Democratic Union CDU pamoja na chama ndugu cha Christian Social Union CSU, umepungua kufuatia ukosoaji wa namna kansela huyo anavyoshughulikia mgogoro wa wakimbizi.
Umaarufu wa Merkel umekuwa ukipungua siku hadi siku, tangu alipofungua mipaka ya Ujerumani kwa wakimbizi mwezi Septemba, kukiwa na wasiwasi kuhusu idadi kubwa iliyokuwa inawasili kila siku na ugumu wanaouongeza juu ya rasilimali za nchi.
Licha ya matumaini ya serikali mjini Berlin kwamba hali ya baridi ingewazuwia wakimbizi kuja Ujerumani, idadi ya watu wanaotafuta hifadhi ilifikia 91,671 mwezi Januari kulingana na maafisa wa serikali. Hii inawakilisha wastani wa wakimbizi 3000 kwa siku.
Chini ya kile kinachojulikana kama makubaliano ya pili kuhusu wakimbizi, wale wanaopatiwa hadhi ya ukimbizi wataendelea kuwa na haki ya kuomba kuleta familia zao kuungano nao. Lakini kwa watu wasio na hadhi kamili ya ukimbizi, hawataruhusiwa kuleta familia zao kwa muda miaka miwili.
Mataifa mapya salaama
Kulingana na gatua hizo mpya, Morocco, Algeria na Tunisia zimeongezwa kwenye orodha ya mataifa salaama, hii ikimaanisha kuwa watafuta hifadhi kutoka mataifa hayo wanaweza kurudishwa kwao chini ya utaratibu mpya wa kushughulikia wakimbizi.
Pendekezo la waziri wa fedha Wolfganga Schäuble, la kutaka wakimbizi wachangie kwenye ada ya mafunzo ya ujumuishaji limejumlishwa pia katika sheria hizo mpya, na kwa hatua hiyo wakimbizi watalipishwa euro 10 ambazo zitakuwa zinatolewa katika fedha zao za msaada kila mwezi kulipia masomo hayo.
Baraza la mawaziri pia limekubaliana kuhusu hatua mpya za kuwarejesha kwao wahamiaji watakaopatikana na hatia ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu, mabadiliko ambayo yametiwa msukumo na madai ya mashambulizi ya kingono na uporaji vilivyodaiwa kufanywa na kundi la wahamiaji katika mkesha wa mwaka mpya mjini Cologne na miji mingine.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpe, DW
Mhariri: Mohammed Khelef