1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sherehe za Ashura huko Karbala, Iraq, zafikia kilele chake

Miraji Othman7 Januari 2009

Washia waadhimisha Ashura, kukumbuka kuuliwa Imam Hussein

https://p.dw.com/p/GT8n
Maandamano ya kuadhimisha Ashura katika mji mtakatifu wa Najaf, IraqPicha: AP

Mamia kwa maelfu ya watu wa madhehebu ya Shia tangu jana walijazana katika barabara za mji wa Karbala, huko Iraq, wengi wao wakijipiga vifua na migongo yao kwa minyonyoro, wakati makumbusho ya Ashura yakianza kufikia kilele chake hii leo. Maeneo matakatifu ya mji huo ulioko kusini mwa Baghdad yamelindwa vikali, huku waumini wa madhehebu ya Kiislamu ya Shia kutoka sehmeu mbali mbali za dunia wakimiminika na kupita kwenye vizuizi vya usalama wakielekea kwenye eneo muhimu la hija yao, kwenye makaburi mawili yaliopambwa, lile la Imam Hussein na la ndugu yake, Imam Abbas.

Ibada hii ya kukumbuka kuuliwa Imam Hussein na majeshi ya khalifa wa madhehebu ya Sunni Yazid hapo mwaka 680 baada ya kuzaliwa Yesu Kristo itafikia kilele huko Karbala hii leo, lakini maandamano ya Ashura, kuadhimisha siku takatifu za kalenda ya madehebu ya Kiislamu ya Shia, yamekuwa yakifanyika nchini kote Iraq mnamo wiki iliopita.

Watu milioni mbili waliwasili jana Karbala, mji ulioko kilomita 110 kusini mwa Baghdad, watu hao wakilindwa na askari wa usalama. Zaidi ya wanajeshi 28,000, wakisaidiwa na polisi, wamepelekwa kuweka usalama katika maadhimisho hayo ya kidini. Akil al-Khazali, gavana wa mkoa wa Karbala, amesema zaidi ya raia wa kigeni 55,000 wameshawasili katika mji huo wakitokea nchi kama vile Iran, Bahrein, Saudi Arabia, Kuwait, Oman, Pakistan na Tanzania.

Jana katika mji huo maandamano ya watu yalipita mabarabarani, na hata watoto, wakifuatana na wapiga ngoma, wote wakijipiga vifua na migongo yao kwa minyonyoro, alama ya kuonyesha huzuni namna Imam Hussein alivouliwa. Hadithi zinasema kwamba Imam Hussein alikatwa kichwa na mwili wake ukakatwakatwa na majeshi ya Yazid.

Mahema na vyumba vidogo vya mbao vikizungushwa na vitambaa vyeusi, huku kukiweko mataa na picha za maimamu wa Kishia, yamesamabaa katika mji wa Karbala. Mahujaji wanaotaka vyakula au msaada wanahudumiwa. Mahujaji kwa kawaida hunywa maji baridi kutoka kwenye bilauri wakikumbuka kiu walichokuwa nacho watu 71 wa familia ya Imam Hussein pale walipoongozwa kama wafungwa katika jangwa la Syria.

Alama gani inayoashiria juu ya kitendo cha mahujaiji wa Ashura huko Karbala kujipiga minyonyoro vifua na migongo yao, hata wengine kutokwa na madamu.

Kwa Washia kushiriki katika maadhimisho ya Ashura ni jambo la pili kwa umuhimu baada ya kuhiji Makkah huko Saudi Arabia. Wengi wanaofika huko wanahisi wametimiza ndoto ya maisha yao.