1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheikh Sharif Ahmed achaguliwa rais wa Somalia

P.Martin31 Januari 2009

Kiongozi wa Kiislamu mwenye msimamo wa wastani,Sheikh Sharif Ahmed,amechaguliwa kuwa rais mpya wa Somalia katika kura iliyopigwa na bunge siku ya Jumamosi.

https://p.dw.com/p/GkQy
Somalia Präsident Sheik Sharif Achmed
Rais mpya wa Somalia Sheikh Sharif Ahmed.Picha: ap

Sheikh Sharif wa chama cha Muungano wa Kuikomboa upya Somali amewashinda wagombea wengine.Katika duru ya pili ya uchaguzi,Sheikh Sharif alimshinda kwa wingi mkubwamhasimu wake Maslah Mohamed Siad Barre.Uchaguzi huo umeitishwa baada ya Abdullahi Yusuf Ahmed kujiuzulu Desemba mwaka jana kufuatia kinyanganyiro cha madaraka kilichozuka kati yake na waziri mkuu Nur Hassan Hussein aliejitoa kugombea uchaguzi wa rais baada ya duru ya kwanza.

Wabunge walikutana Djibouti kupiga kura kwa sababu ya ukosefu wa usalama nchini Somalia.Ni matumaini yao kuwa rais aliechaguliwa atafanikiwa kuwatenga au kuwashawishi waasi wenye misimamo mikali kuiungana mkono serikali mpya.Rais Ahmed aliongoza chama cha mahakama za Kiislamu kilichofanikiwa kuleta aina ya utulivu katika mji wa Mogadishu na katika maeneo mengi kusini mwa Somalia katika mwaka 2006 kabla ya kutimuliwa madarakani na vikosi vya Ethiopia vilivyopelekwa kuisaidia serikali ya mpito ya Somalia.

Wachambuzi wanasema,Sheikh Sharif Ahmed ana nafasi nzuri ya kuwaunganisha Wasomali kwa sababu ya mizizi yake ya Kiislamu na vile vile anaungwa mkono na bunge.Hata hivyo si rahisi kupatanisha watu wapatao milioni10 nchini Somalia na kukomesha umwagaji damu unaoendelea tangu miaka 18.Zaidi ya raia 16,000 wameuawa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na idadi ya wanamgambo waliopoteza maisha yao katika mapigano na vikosi vya serikali na washirika Ethiopia haijulikani.Mapigano hayo yamesababisha kiasi ya watu milioni moja kupoteza makazi yao huku theluthi moja ya umma ukitegemea msaada wa chakula.Kwa mujibu wa mashirika ya misaada,hali inayokutikana Somalia ni miongoni mwa maafa mabaya kabisa ya binadamu yanayoshuhudiwa duniani.