1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulizi la mabomu laua zaidi ya watu 50 Algeria

11 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CaJ7

ALGIERS.Zaidi ya watu 50 wameuawa nchini Algeria huku wengine kadhaa wakijeruhiwa baada ya mabomu mawili kulipuka katikati ya mji mkuu Algiers.

Miongoni mwa waliyouawa ni wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa ambao moja ya mabomu hayo lililipuka karibu na ofisi zake, huku lingine likipuka ndani ya basi lililokuwa na wanafunzi wa chuo kikuu karibu na jengo la Mahakama Kuu ya Algeria.

Bomu hilo lililipuka karibu na ofisi ya Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR ambazo ziko katika maeneo yanayokaliwa na raia wengi wa kigeni.

Mmoja wa maafisa wa shirika hilo amesema kuwa mpaka sasa wafanyakazi 12 hawajulikani walipo na inahofiwa kuwa wamekufa katika mlipuko huo.

Kuna hisia kuwa huenda ofisi za shirika hilo ndiyo zilikuwa lengo la shambulizi hilo.

Nchi kadhaa zimelaani shambulizi hilo zikiwemo Marekani na Umoja wa Ulaya.

Hakuna kikundi chochote mpaka sasa kilichodai kuhisika na shambulizi hilo.