1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulizi la bomu lawaua kiasi ya watu 15 Abuja,Nigeria

2 Mei 2014

Shambulizi la bomu katika kiunga cha mji mkuu wa Nigeria, Abuja limewaua watu wasiopungua19 na kuwajeruhi wengine kadhaa wiki moja kabla ya mji huo kuwa mwenyeji wa kongamano la kiuchumi duniani

https://p.dw.com/p/1BsHw
Picha: dpa

Shambulizi hilo la jana jioni lilitokea katika mji wa Nyanya viungani mwa Abuja karibu na kulikotokea shambulizi jingine la tarehe 14 mwezi uliopita ambalo liliwaua kiasi ya watu 75.

Moto ulizuka katika eneo la mkasa ambalo lilizagaa miili na kutapaka damu huku ving'ora vya magari ya kubeba wagonjwa vikisika katika eneo hilo yalipokwenda kuwakimbiza majeruhi hospitalini.

Mripuko huo ulitokea karibu na kituo cha mabasi huku watu wengi wakisubiri kupanda magari ya umma.Kufikia sasa hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulizi hilo lakini inashukiwa kuwa limefanywa na kundi la waasi la Boko Haram ambao wamedai kuhusika na shambulizi la mwezi uliopita mjini humo.

Boko Haram yaleta mashambulizi katika mji mkuu

Hili ni shambulizi la pili kufanyika Abuja katika kipindi cha miaka miwili.Boko Haram imekuwa ikifanya mashambulizi yake katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo lakini sasa inahofiwa wameanza kutanua uasi wao hadi miji mikuu.

Watu wakiandamana Abuja wakitaka serikali kuwaoko wasichana waliotekwa nyara
Watu wakiandamana Abuja wakitaka serikali kuwaoko wasichanaPicha: DWU. Abubakar Idris

Shambulizi hilo ni fedheha kwa Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ambaye anaonekana kushindwa kukabiliana na kundi hilo la waasi.Serikali ilikuwa imetangaza kuwa itaimarisha usalama maradufu katika mji huo mkuu huku ikijiandaa kuwa mwenyeji wa jukwaa la kiuchumi duniani linalotarajiwa kuanza tarehe saba wiki ijayo hadi tarehe tisa.

Nigeria imatangaza kuwa polisi na wanajeshi 6,000 watashika doria mjini Abuja wakati wa mkutano huo unaotarajiwa kuhudhuriwa na waziri mkuu wa China Li Keqiang,viongozi wa nchi za Afrika na watu wengine mashuhuri kutoka mataifa ya kigeni.

Marekani kusaidia kuwaokoa wasichana waliotekwa nyara

Serikali ya Nigeria imeshutumiwa vikali kutokana na kushindwa kushughulikia vitisho kutoka kwa Boko Haram huku makundi ya kutetea haki za binadamu na jamaa za wasichana takriban 200 waliotekwa nyara mwezi uliopita wakiandamana katika miji mbali mbali kuishurutisha serikali kuchukua hatua zaidi kuwapata na kuwaokoa wasichana hao.

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan
Rais wa Nigeria Goodluck JonathanPicha: Pius Utomi ekpei/AFP/Getty Images

Marekani imetangaza kuwa itaisaidia Nigeria kuwatafuta wasichana hao ambao hawajulikani waliko huku kukiwa na taarifa kuwa huenda wameozwa kwa waasi walioko katika nchi jirani za Chad na Cameroon.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za kigeni wa Marekani Marie Harf amesema serikali za nchi hizo mbili zimefanya mazungumzo kuona ni kipi Marekani inaweza kufanya kuunga mkono juhudi za kuwaokoa wasichana hao wa shule ya upili iliyoko katika mji wa Chibok.

Kundi la maseneta wa Marekani limelaani kutekwa nyara kwa wasichana hao na kuihimiza serikali ya Marekani kusaidia katika juhudi za kuwaokoa.Seneta Chris Coons wa jimbo la Delaware na ambaye ni mwenyekiti wa kamati ndogo kuhusu masuala ya Afrika amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kuhakikisha wasichana hao wamerejeshwa kwa familia zao na kukabiliana na Boko Haram ambao wanaendeelea kuwa kitisho katika kanda hiyo.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/ap

Mhariri: Daniel Gakuba