Shambulio la Nairobi na jibu la walimwengu
24 Septemba 2013Shambulio la jumamosi katika jengo la biashara la Westgate Mall,lililofuatiwa na utekaji nyara,limefanywa na wanamgambo kati ya 10 na 15.Hayo ni kwa mujibu wa maafisa wa serikali ya Kenya.Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha PBS waziri wa mambo ya nchi za nje wa Kenya Amina Mohammed alisema "wamarekani wawili au watatu na raia mmoja wa Uingereza ni miongoni mwa wanamgambo.
Kwa maoni yake,wanamgambo hao ni vijana ambao umri wao ni kati ya miaka 18 na 19 wenye asili ya kisomali au kiarabu,lakini wanaishi Marekani katika jimbo la Minnesota na kwengineko.
Wanamgambo wa kisomali wa wakigeni
Katika mkutano na waandishi habari,waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Joseph Ole Lenku alisema wanamgambo wanaonyesha ni wanaume hata kama baadhi yao wamevalia kama wanawake.
Afisa mmoja wa idara ya upelelezi na wanajeshi wawili wa Kenya wameliambia lakini shirika la habari la Reuters kwamba bibi mmoja mzungu ni miongoni mwa wanaharakati waliokutikana wameuwawa.Hoja hizo zinashadidia uvumi kwamba pengine bibi huyo ni yule mjane wa mmojawapo wa waasisi wa mashambulio ya msimu wa kiangazi mwaka 2005 mjini London.
Akijulikana kwa jina la "Mjane mweupe" na vyombo vya habari vya Uingereza,Samantha Lewthwaite anasakwa kwa madai ya kuhusika na njama ya kutaka kushamabulia hoteli na mikahawa nchini Kenya.Alipoulizwa kama kama maiti hiyo ya mwanamke ni ya Samantha Lewthwaite,afisa wa idara ya upelelezi amejibu tu:"hawajui."
Korti kuu ya kimataifa mjini The Hague iko tayari kushirikiana na Kenya
Uingereza inapinga kusema chochote kuhusu ripoti kama bibi huyo ni miongoni mwa wanamgambo wanaoendelea kushikilia mateka katika jengo hilo la biashara la Westgate Mall mjini Nairobi.Hata hivyo msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP tunanukuu"Tumesikia kilichosemwa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Kenya bibi Amina Mohammed na tunaendelea kushirikiana kwa dhati na viongozi wa Kenya na kuwasaidia katika uchunguzi wao" amesema na kuongeza Uingereza itafanya kila liwezekanalo kuisaidia Kenya ili wote wanaohusika na shambulio hilo la kinyama wafikwishe mahakamani."Mwisho wa kumnukuu msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Uingereza.
Nae mwendesha mashtaka mkuu wa korti ya kimataifa ya uhalufu mjini The Hague Fatou Bensouda amesema yuko tayari kushirikiana na Kenya ili kuwafikisha mahakamani wanaohusika shambulio lililoangamiza maisha ya watu katika jengo la biashara mjini Nairobi.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters,AFP/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman