1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la Münster na mwongozo wa wahafidhina magazetini

Oumilkheir Hamidou
9 Aprili 2018

Shambulio la Münster na dhana zilizoenezwa mtandaoni na mbunge wa chama cha AFD, na uamuzi wa chama cha Christian Democratic Union CDU kufuata mwongozo wake wa jadi ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/2viJC
Deutschland Münster Attacke mit Campingbus | Gedenken Horst Seehofer & Armin Laschet
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kusch

Tunaanzia Münster ambako hata kabla ya uchunguzi kukamilika kuhusu chanzo cha shambulio lililoangamiza maisha ya watu wawili waliokuwa wameketi pamoja na wenzao kuota juwa mbele ya mkahawa mmoja katika mji huo wa kale, uvumi ulikuwa tayari umeshaenea mtandaoni kuashiria "shambulio la kigaidi la wafuasi wa itikadi kali ya dini ya Kiislam". Gazeti la "Weser-Kurier" linamkosoa mbunge wa chama cha "Chaguo Mbadala kwa Ujerumani", Beatrix von Storch aliyejaribu kulitumia tuko la Münster kwa masilahi ya kisiasa. Gazeti linaandika: "Afadhali angeonyesha  moyo wa huruma na huzuni , lakini mwanasiasa wa AfD Beatrix von Storch anaonyesha kuvutiwa zaidi na masilahi ya kisiasa."Tutaweza" aliandika katika mtandao wake wa twitter, mwanasiasa huyo, dakika 20 tu baada ya tukio hilo la kutisha la Münster, akifungamanisha neno hilo na lile alilowahi kulitamka kansela Angela Merkel. Kwa namna hiyo alikuwa anataka kuleta uwiano kati ya itikadi kali ya dini ya Kiislam na shambulio hilo, bila ya kupata  ushahidi wowote wa alichokua akikieneza."

Sura mbili tofauti za Ujerumani

Mhariri wa Weser-Kurier anasema watu mfano wa bibi von Storch hawahitaji ushahidi, muhimu kwao ni kueneza dhana tu. Gazeti la "Rhein-Zeitung" linasema shambulio la Münster limepelekea kuibuka Ujerumani ya sura mbili tofauti. Gazeti hilo linaendelea kuandika: "Shambulio la kutisha lililomwaga damu mjini Münster limedhihirisha jinsi Ujerumani ilivyogawika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni ile ya utu na huruma na sehemu ya pili ni ile ya dharau na kutothamini utu. Kwa miongo kadhaa, jamii ilikuwa ikihuzunika na kushituka tukio kama hilo linapojiri. Lakini hisia mbadala zinaonyesha zimeingia mpaka huko hivi sasa.Tukio lililofanywa na mjerumani aliyekuwa na matatizo ya kiakili linataka kugeuzwa shambulio la kigaidi la itikadi kali ya dini ya Kiislam. Salama wakaazi wa Münster wameonyesha mfano mzuri unaozidi kuimarisha sifa ya Ujerumani: wametoa damu kusaidia badala ya umbeya."

Mwongozo asilia wa kihafidhina kwa wahafidhina

Mvutano umezuka ndani ya chama cha Christian Democratic Union CDU cha kansela Angela Merkel kuhusu suala kama kiendelee kufuata mkondo wa siasa za wastani za kihafidhina au kirejee katika mkondo wake wa jadi wa kihafidhina. Mwishoni mwa wiki suala hilo lilizushwa viongozi wa CDU na wale wa chama ndugu cha CSU walipokutana Schwetzingen. Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linaandika: "Zilzala haijapiga katika mkutano huo wa Schwetzingen. Wafuasi wa Umoja wa kimaadili, tawi la wafuasi wa siasa za kihafidhina ndani ya vyama ndugu vya CDU/CSU, hawana njia nyengine isipokuwa kuridhika na yale haba waliyoyapata. Malalamiko ya wahafidhina si ya leo, yameanza tangu kansela Merkel alipokabidhiwa hatamu za uongozi wa chama hicho. Miaka 18 iliyopita."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga