1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la kigaidi mjini Tripoli laua 12

Oumilkheir Hamidou
2 Mei 2018

Watu wasiopungua 12 wameuwawa na saba kujeruhiwa kufuatia shambulio dhidi ya makao makuu ya halmashauri kuu ya uchaguzi HNEC mjini Tripoli.

https://p.dw.com/p/2x3aJ
Libyen Selbstmordanschlag in Tripolis
Picha: Reuters/Al Nabaa Channel

 

Watu wanne walioshamiri silaha walilihujumu jengo la halmashauri kuu ya Uchaguzi HNEC. Afisa wa ngazi ya juu wa usalama Mohammed al-Damja amewaambia waandishi habari magaidi hao wamewauwa walinzi kabla ya kuwafyetulia risasi watu waliokuwemo ndani ya jengo hilo.

Magaidi wasiopungua wawili walijiripua vikosi vya usalama vilipowasili. Makao makuu ya halmashauri kuu ya uchaguzi imeteketea vibaya sana kwa moto.Vikosi vya usalama vinadhibiti hali ya mambo hivi sasa.

Wafuasi wa itikadi kali wa dola la kiislam IS wamedai kuhusika na shambulio hilo lililoangamiza maisha ya watu wasiopungua 12 na wengine saba kujeruhiwa.

Kwa mujibu wa mashahidi, risasi na mizinga isiyopungua miwili iliyofyetuliwa ilisikika ndani ya jengo la halmashauri kuu ya uchaguzi lililozungushwa senyenge ili kuwazuwia waandishi habari na wambeya kulijongelea.

Katika ripoti yake serikali ya umoja wa taifa imelaani "shambulio la kigaidi" ambalo inasema "halitoizuwia serikali ya umoja wa taifa kuendelea kuiunga mkono halmashauri kuu ya uchaguzi na kuheshimu utaratibu wa kidemokrasi wa kuitisha uchaguzi kwaajili ya mustakbali mwema wa Libya."

Jenerali Khalifa Haftar anaeunga mkono serikali iliyoko mashariki mwa Libya
Jenerali Khalifa Haftar anaeunga mkono serikali iliyoko mashariki mwa LibyaPicha: Reuters/E. Omran

Miito ya jumuia ya kimataifa kwa walibya

Tume ya Umoja wa mataifa nchini Libya imelaani pia shambulio hilo."Mashambulio kama hayo ya kigaidi hayatowazuwia walibya kusonga mbele katika utaratibu wa kuimarisha umoja wa taifa na ujenzi wa taifa linaloheshimu sheria na taasisi zake" tume ya umoja wa mataifa nchini Libya-Manul imesema katika taarifa yake kupitia mtandao wa twitter.Tume hiyo ya umoja wa mataifa imewatolea wito maafisa wa serikali nchini Libya wawaandame na kuwafikisha mahakamani haraka iwezekanavyo waliohusika na mashambulio hayo.

LIbya inakabwa na vurugu tangu serikali ya Muammar Gaddafi ilipoporomoshwa mwaka 2011. Serikali mbili zinapigania madaraka nchini humo; Serikali ya umoja wa taifa GNA inayotambuliwa na jumuia ya kimataifa na yenye makao yake makuu mjini Tripoli na serilali ya pili ni ile iliyoko mashariki mwa Libya na kuungwa mkono na kiongozi matata wa kijeshi Khalifa Haftar.

Jumuia ya kimataifa inawashinikiza viongozi wa nchi hiyo waitishe uchaguzi mwaka huu wa 2018 wakitaraji kurejesha hali ya utulivu katika nchi hiyo tajiri kwa mafuta.

Shambulio la Benghazi january 24 mwaka huu wa 2018
Shambulio la Benghazi january 24 mwaka huu wa 2018Picha: Reuters

Hali hairuhusu uchaguzi kuitishwa

Lakini hakuna bado tarehe iliyopangwa ya kuitisha chaguzi hizo katika wakati ambapo zitabidi zitanguliwe na kura ya maoni kuhusu mswaada wa katiba na kubuniwa sheria mpya ya kupiga kura.

Wapiga kura milioni mbili na laki nne  kati ya wananchi milioni 6 wa Libya wameshajiandikisha katika orodha za halmashauri kuu ya uchaguzi.

Halmashauri kuu ya uchaguzi inatajwa kuwa miongoni mwa taasisi zinazoaminika na huru nchini Libya. Imeshasimamia uchaguzi mara mbili, mwaka 2012 na mwaka 2014. Mwezi Marchi uliopita shirika linalopigania haki za binaadam Human Rights Watch liliashiria hali namna ilivyo nchini LIbya hairuhusu kuitishwa uchaguzi huru na wa uwazi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman