Shambulio kubwa la kigaidi katika msikiti nchini Pakistan
4 Desemba 2009Watu wawili waliojitolea mhanga walijiripuwa wenyewe katika msikiti, na wengine wawili wakawafyetulia risasi watu waliokuwa wakifanya ibada karibu na makao makuu ya jeshi la nchi hiyo hii leo punde baada ya Sala ya Ijumaa. Si chini ya watu 40 waliuwawa, wakiwemo maafisa wa jeshi.
Watu wengi wanaokwenda katika msikiti huo ni maafisa wa jeshi katika mji wa Rwalpindi, mji ambako maafisa wakuu wengi wa jeshi wanaishi, na ni masafa ya muda wa dakika thalathini tu kwa gari kutoka mji mkuu wa Islamabad. Shambulio hilo limefanyika katika eneo ambalo linatajwa ndilo lenye usalama mkubwa kabisa katika Pakistan, hivyo kuwa ni mtihani kwa dola. Kituo cha televisheni kilisema watu waliuwawa, huku wenyewe wakijiona. Kulikuwa watoto miongoni mwao ambao walikwenda kusali pamoja na baba zao. Pia kulikuweko watu waliozeeka na ambao wamestaafu kutoka jeshi. Msemaji wa jeshi, Meja-jenerali Athar Abbas, alisema kuna meja-jenerali wa jeshi aliyeuwawa. Meja-Jenerali Abbas alisema jumla ya watu waliouwawa ni 36; magaidi wanne pia wameuwawa.
Jeshi la Pakistan linapigana na wapiganaji wa Kitaliban ambao wanaulaumiwa kuripua mabomu yaliowauwa mamia ya watu tangu hujuma kuanzishwa dhidi yao katika Kusini mwa jimbo la Waziristan mwezi Oktoba mwaka huu. Pakistan, ilio na mabomu ya ikinyukliya, inazidi kubinywa na Marekani, ikitakiwa iwang'oe Waislamu wenye siasa kali ambao wanaendesha harakati zao katika maeneo ya mpakani. Marekani inasema kwa kufanya hivyo, Pakistan itasaidia pia katika vita dhidi ya Wataliban wa Afghanistan.
Waziri wa mambo ya ndani, Rehman Malik, aliwaambia waandishi wa habari kwamba washambuliaji wawili wa kujitolea walijiripuwa ndani ya msikiti, huku wengine wawili wakiwa wanafyetua risasi nje ya msikiti. Watoto kumi ni miongoni mwa watu waliokufa. Alisema washambuliaji hao sio tu ni maadui wa Uislamu, lakini ni maadui wa nchi pia. Wanataka kukimaliza kizazi kinachokuja. Polisi walisema washambuliaji waliwasili hapo wakiwa katika gari la aina ya Toyota.
Imamu wa msikiti punde alimaliza hotuba yake kwa kusema Allahu Akbar, pale mripuko ulipowatikisa watu waliokuwa wakiendesha ibada katika Msikiti wa Parade Lane. Shahidi mmoja alisema punde walipomaliza sala, walisikia mripuko na milio ya risasi, akiwaona watu waliojeruhiwa wakilala katika uwanja wa msikiti.
Michafuko hii itambinya Rais Asif Ali Zardari achukuwe hatua zaidi ili kukabiliana na kitisho cha uasi wa Wataliban walio wakaidi. Lakini rais huyo anazidi kutopendwa na wananchi, serekali yake ikiwa dhaifu na kutosikilizana na jeshi lenye nguvu.
Akielezea mkakati wake kuelekea Afghanistan, katika hotuba yake ya jumanne iliopita, Rais Barack Obama wa Marekani aliiomba Pakistan ipigane na saratani ya siasa kali, na akasema Marekani haitaistahamilia Pakistan iruhusu kutumiwa ardhi yake kuwa pepo ya watu wenye siasa kali. Ombi hilo ni taabu kutekelezeka katika nchi ambako hisia na wasiwasi dhidi ya Marekani ni mkubwa. Wengi wa wananchi wa Pakistan wanasema nchi yao isipigane vita vya Marekani dhidi ya watu wenye siasa kali. Kushindwa Afghanistan kunaweza kukachafua kipindi hiki cha urais wa Barack Obama.
Naye waziri mkuu wa Uengereza, Gordon Brown, ambaye alifanya wiki hii mazungumzo na waziri mkuu wa Pakistan, Yousuf Raza Gilani, mjini London amepeleka simu ya rambi rambi kwa Rais wa Pakistan akilaani shambulio hilo baya, akisema Uengereza inasimama bega kwa bega na Pakistan katika kupambana na kitisho cha ugaidi.
Mwandishi: Miraji Othman/Reuters/AP
Mhariri: Mohammed Abdulrahman