Serikali zachukua hatua kuzuia wimbi jipya la COVID-19
28 Julai 2020Mataifa ya Ulaya yamejikuta njia panda wakati yanajaribu kurekebisha athari za kiuchumi za janga la virusi vya corona kwa kufungua tena shughuli za kawaida ikiwemo utalii huku yakijilinda na wimbi jipya la maambukizi ya COVID-19.
Sekta ya utalii ya Uhispania jana ilipata baada ya moja ya kampuni kubwa ya utalii kusitisha mipango ya safari kwa raia wa Uingereza kufuatia uamuzi wa serikali mjini London wa kurejesha sharti la kuwaweka watu karantini kwa muda wa wiki mbili pindi wanaporejea kutoka nje.
Kampuni mashuhuri ya utalii ya TUI imetangaza kufuta safari zote za watalii wa Uingereza kuanzia Agosti 9 ikisema kanuni ya kuwaweka watu karantini itazuia walio wengi kufanya safari nje ya Uingereza.
Ujerumani kuwapima kwa lazima wasafiri
Nchini Ujerumani serikali itaanzisha upimaji wa lazima wa COVID-19 kwa wasafiri wote kutoka maeneo yaliyo na hatari kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona kufuatia kuongezeka kwa visa vya COVID-19 kwenye miji inayotembelewa kwa wingi na watalii.
Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn ameliambia shirika la habari la DPA kuwa atatumia mamlaka aliyonayo kuweka utaratibu wa lazima wa kufanyika vipimo kwa lengo la kuzuia watu wanaotoka nje kusambaza virusi nchini Ujerumani.
Huku idadi ya visa vya COVID-19 ikipanda nchini Ujerumani, mkuu wa utumishi wa ofisi ya Kansela Angela Merkel, Helge Braun ametoa wito kwa umma kuheshimu kanuni za usafi na kujitenga kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.
"Tunapaswa kujituma ili kupunguza tena maambukizi, na yanapaswa kuwa kwa kiwango cha chini sana mwishoni mwa majira ya kiangazi, kwa sababu, tunachojua, ni rahisi kwetu kupunguza maambukizi wakati wa kiangazi kuliko msimu wa mapukutiko au wa baridi, kama ambavyo shirika la afya la WHO lilivyoainisha tena hivi leo." amesema Braun.
Mshauri wa usalama wa taifa nchini Marekani aambukizwa virusi
Huko nchini Marekani, Ikulu ya White House imetangaza kwamba afisa mwingine wa ngazi ya juu ambaye ni mshauri wa usalama wa taifa Robert O´Brien ameambukizwa virusi vya corona.
Hadi jana jioni Marekani ndiyo taifa lililoathiriwa vibaya na virusi vya corona baada ya kuongezeka visa vipya 57,000 na kurikodi idadi ya vifo 147,588 kwa mujibu wa takwimu za chuo kikuu cha Johs Hopkins.
Mjini Hong Kong serikali imearifu kuwa sasa ni lazima kwa watu wote kuvaa barakoa wawapo kwenye maeneo ya umma kama juhudi mpya ya kupambana na wimbi jipya la maambukizi ya virusi.
Katibu mkuu kiongozi wa serikali ya mji huo Matthew Cheung amesema hali ya janga la COVID.19 ni mbaya mjini Hong Kong kwa hivyo pamoja na maelekezo ya kuvaaa barakoa, mikusanyiko ya watu wanaozidi wawili imezuia kwenye maeneo yote ya wazi na mikahawa.