Serikali ya Yemen na waasi watia saini makubaliano ya amani
6 Novemba 2019Mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia ameyasifu kuwa makubaliano hayo kuwa ni hatua kuelekea suluhisho pana la kisiasa na kuweza kumaliza mzozo huo wenye ncha nyingi.
Mkwamo ulifungua eneo lingine katika vita vya zaidi ya miaka minne na kutia ufa katika muungano unaoongozwa na saudi Arabia unaopigana na vuguvugu la Wahouthi ambalo liliiondoa serikali inayoongozwa na rais Abd-Rabbo Mansour Hadi kutoka mji mkuu , Sanaa, upande wa kaskazini mwa nchi hiyo mwishoni mwa mwaka 2014.
Balozi wa Saudi Arabia nchini Yemen aliwaambia waandishi habari kuwa makubaliano hayo , yaliyofikiwa baada ya zaidi ya mwezi mmoja wa mazungumzo ya ana kwa ana katika mji mkuu wa Saudi Arabia , utashuhudia kundi hilo linalotaka kujitenga la kusini mwa Yemen linalojulikana kama Southern Transitional Council, STC, likijiunga na baraza jipya la mawaziri pamoja na watu wengine wa kusini na makundi yote yenye silaha yatawekwa chini ya udhibiti wa serikali.
Mwanamfalme Mohammed bin Salman alisema.
"Makubaliano haya yatafungua , uaminifu, mazungumzo mapana kati ya makundi ya Wayemeni ili kufikia suluhisho la kisiasa ambalo litafikisha mwisho mzozo huu wa Yemen na kuilinda Yemen, pamoja na kila kitu kilichomo, dhidi ya wale ambao hawaitakii mema. tunamuomba Mungu abariki juhudi zetu na kuona kuwa zinafanikiwa, kwa ajili ya nchi zetu na watu wetu."
Mwanzo mzuri
Rais wa Marekani Donald Trump ameyasifu makubaliano hayo kupitia ukurasa wa Twitter kwa kusema , "Mwanzo mzuri sana ! tafadhali fanyeni kazi wote kupata makubaliano ya mwisho."
Saudi Arabia imekuwa ikijaribu kutatua mkwamo huo katika kuweka mwelekeo mpya kwa muungano unaopambana na vuguvugu la wahouthi linaloungwa mkono na Iran katika mpaka wa kusini.
Majeshi yanayotaka kujitenga , yakisaidiwa na mshirika muhimu wa Saudi Arabia , Umoja wa Falme za Kiarabu, ni sehemu ya muungano wa Waislamu wa madhehebu ya Sunni ambao umeingilia kati nchini Yemen Machi mwaka 2015 dhidi ya Wahouthi ambao wanaushikilia mji mkuu wa Sanaa pamoja na mingi ya miji mikubwa.
Lakini kundi la STC , ambalo linataka utawala wa ndani katika eneo la kusini na kuwa na sauti katika Yemen ya hapo baadae, limeigeuka serikali ya Hadi mwezi Agosti, na kukamata mji wake mkuu wa bandari ya kusini ya Aden na kujaribu kupanua himaya yake upande wa kusini.