Serikali ya upinzani kuton'gan'gania madaraka Libya
1 Aprili 2016Utawala uliojitangazia serikali wenye makao yake mjini Tripoli Libya umesema hautong'ang'ania madaraka lakini utapinga kwa njia ya amani serikali ya umoja wa kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ambayo wajumbe wake wamewasili katika mji mkuu wa nchi hiyo wiki hii.
Mataifa ya magharibi yanataraji serikali hiyo ya umoja wa kitaifa itaomba msaada wa kigeni kupambana na kundi la wanamgambo wa Dola la Kiislamu, kukabiliana na wimbi la wahamiaji wanaokimbilia Ulaya kupitia Libya na kuanza tena uzalishaji wa mafuta ili kuinuwa uchumi wa nchi hiyo.
Lakini serikali hiyo mpya ambayo imekuwa na vikao vyake vya kwanza mjini Tripoli hapo Alhamisi katika kituo cha wanamaji chenye ulinzi mkali imeshindwa kuungwa mkono na serikali mbili hasimu nchini Libya pamoja na mabunge yao, moja ikiwa na makao yake mjini Tripoli na nyengine mashariki mwa nchi hiyo.
Kiongozi wa serikali ilioko Tripoli ya Uokovu wa Taifa Khalifa Ghwell amepinga vikali kukabidhiwa madaraka kwa serikali hiyo kwa njia yoyote ile. Lakini taarifa iliochapishwa usiku wa manane hapo Alhamisi katika ukarasa wa mtandao wa serikali hiyo kauli yake haikuwa kali kwa kusema kwamba "upinzani utakuwa kwa njia ya amani na kisheria bila ya matumizi ya nguvu au uchochezi wa ghasia."
Taarifa hiyo imesema: "Hatuton'gan'gania madaraka". Kiongozi wa serikali hiyo amewataka wanamapinduzi, mashirika ya kiraia na makarani waandamizi wapewe fursa ya kuchukuwa hatua zinazohitajika kuepuka umwagaji damu na kupata ufumbuzi kwa mzozo wa Libya.
Kuungwa mkono kwa serikali mpya
Katika kile kinachoonekana kama ni kuipa nguvu serikali hiyo mpya ya umoja wa kitaifa na uongozi wake au Baraza la Urais miji kumi ilioko magharibi mwa Libya imesema inakaribisha na kuunga mkono kuwasili kwa serikali hiyo.
Imesema serikali za mitaa za mwambao wa magharibi zinatambuwa fika kwamba hiki ni kipindi muhimu na kutowa wito kwa wananchi wa Libya kuwa kitu kimoja katika kuiunga mkono Serikali ya Makubaliano ya Taifa.
Umoja wa Ulaya umezuwiya mali za Ghwell na maspika wa mabunge ya Tripoli na mashariki ya nchi hiyo kutokana dhima zao katika kuikwamisha serikali hiyo ya umoja wa kitaifa. Vikwazo hivyo vinaanza kutumika kuanzia Ijumaa.
Kuanza kuchukuwa udhibiti
Baraza la Urais la serikali hiyo mpya lenye wajumbe saba linajaribu kuchukuwa udhibiti wa taasisi zilioko Tripoli na kuungwa mkono na makundi mengi ya wapiganaji yalioko katika mji mkuu huo.
Afisa katika wizara ya mambo ya nje mjini Tripoli amesema vikosi vya usalama vilivyo tiifu kwa Baraza la Urais vimedhibiti jengo la wizara hiyo na kwamba waziri ambaye aliteuliwa awali na serikali ya Uwokovu wa Taifa ameondoka kwa amani.
Mji wa Tripoli kwa kiasi kikubwa umekuwa kwenye utulivu tokea kuwasili kwa wajumbe wa Baraza la Urais la serikali mpya hapo Jumatano. Walikwenda Tripoli kwa kutumia meli wakitokea Tunisia baada ya wapinzani kufunga anga ya mji mkuu huo kuwazuwiya kuingia.
Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef