1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya yashindwa kuanza kazi

7 Aprili 2016

Matumaini ya serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya kuanza kazi rasmi katika mji wa Tripoli yameingia doa baada ya kiongozi wa utawala hasimu uliokuwepo mjini Tripoli kukataa kuachia madaraka.

https://p.dw.com/p/1IRHJ
Waziri Mkuu wa serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya Fayez al-Sarraj
Waziri Mkuu wa serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya Fayez al-SarrajPicha: picture-alliance/dpa

Waziri Mkuu wa serikali isiyotambulika ya Tripoli Khalifa Ghweil aliwataka mawaziri wake kutojiuzulu hali ambayo inaibua utata na kuleta mkanganyiko kuhusiana na kauli yake ya awali ambapo alisema serikali hiyo inayojulikana kama serikali ya uwokozi ilikua tayari kujiuzulu.

" Kwa kuzingatia masilahi ya umma mnapaswa kuendelea na kazi kama kawaida kwa mujibu wa sheria" alisema kiongozi huyo na kutishia kuwashitaki wale wote watakaonekana kushirikiana na serikali hiyo mpya.

Sababu za kubadili msimamo wake wa awali hazikuweza kujulikana mara moja ingawa huenda kukawepo na mgawanyiko kuhusiana na suala hilo ndani ya serikali hiyo iliyoudhibiti mji wa Tripoli miaka miwili iliyopita na kuilazimisha serikali inayotambuliwa kimataifa kuondoka.

Juhudi za Umoja wa Mataifa za kumaliza mzozo zaonekana kukwama

Hatua hiii inaonekana kukwamisha juhudi za Umoja wa Mataifa za kujaribu kumaliza mzozo uliosababisha mgawanyiko mkubwa katika utawala wa nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano sasa ikiwa ni siku moja kabla ya Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro huo Martin Kobler kuwasilisha taarifa yake katika Umoja wa Mataifa kuhusiana na maendeleo ya jitihada hizo.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Libya Martin Kobler
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Libya Martin KoblerPicha: picture alliance/AA/A. Landoulsi

Bado kulikuwa hakujawepo na kauli kutoka kwa Waziri Mkuu anayetarajiwa kuongoza serikali ya Umoja wa kitaifa Fayez al- Sarraj ambaye alikuwa tayari ameanza kuimarisha udhibiti wake katika hazina ya nchi hiyo pamoja na taasisi zake.

Serikali hiyo ya uwokozi inayoongozwa na bwana Gheil ilifanikiwa kuudhibiti mji wa Tripoli katikati ya mwaka 2014 kwa msaada wa wanamgambo na kuilazimisha serikali inayoungwa mkono na Jumuiya ya kimataifa kukimbilia upande wa mashariki mwa nchi hiyo.

Serikali ya Umoja wa kitaifa iliundwa mwezi Desemba mwaka jana chini ya makubaliano ya kugawana madaraka yaliyofikiwa kwa pamoja na wabunge kutoka pande za kisiasa nchini humo zinazohasimiana.

Kiongozi wa serikali ya Umoja wa Kitaifa Fayez al Sarraj aliwasili katika mji wa Tripoli akiwa na ulinzi mkali na kuweka makao yake katika kituo cha jeshi la majini na alikuwa tayari ameanza mikakati ya kuanza utendaji kazi wa serikali ya hiyo ya Umoja wa Kitaifa.

Jumuiya ya kimataifa tayari imeziomba pande zinazopigana nchini Libya kuungana chini ya serikali ya Umoja wa kitaifa, ambayo ni muhimu ili kupambana na makundi ya jihadi yanayojipanua na watu wanaofanya biashara haramu katika taifa hilo la Afrka ya Kaskazini.

Hatua ya serikali hiyo ya uwokozi kubadili msimamo wake wa awali inaonyesha kukwamisha juhudi za kumaliza uhasama wa kisiasa nchini humo licha ya awali kutoa kauli ya kuwa itajiuzulu ili kuepusha umwagaji damu na pia mgawanyiko.

Waziri Mkuu wa Serikali ya uwokozi ya Tripoli Khalifa Al-ghwell
Waziri Mkuu wa Serikali ya uwokozi ya Tripoli Khalifa Al-ghwellPicha: picture-alliance/AA/H. Turkia

Mapema hapo jana Waziri wa mambo ya nje wa Italia Paulo Gentiloni alisema hatua iliyokuwa imefikiwa hivi karibuni ilikuwa inaleta matumaini katika kuelekea kuwa na taifa la Libya lililo salama. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Italia ambayo Libya ilikuwa chini ya himaya ya nchi hiyo wakati wa kipindi cha utawala wa kikoloni aliahidi serikali ya Italia kuipa ushirikiano wa kutosha serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa.

Awali Waziri Mkuu wa serikali ya Umoja wa Kitaifa aliagiza wizara zote pamoja na taasisi za serikali kuheshimu mamlaka yake ikiwa ni pamoja na kutoa maagizo kwa benki kuu na taasisi ya ukaguzi wa mahesabu nchini humo kuzuia akaunti zote za serikali isipo kuwa tu zile ambazo zinahusika na malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga