Uchaguzi utakaoamua hatma ya Catalonia waanza
21 Desemba 2017Kulingana na utafiti wa kura ya maoni uchaguzi huu utakuwa na ushindani mkali kati ya vyama vinayotaka kujitenga vya Catalonia na kambi za kikatiba wakati Uhispania ikisubiri kwa hamu kuona iwapo vyama hivyo vinavyotaka kujitenga vitapata wingi wa kura bungeni na kuunda serikali ya muungano.
Aidha raia milioni 5.5 wa Catalonia wamesajiliwa kupiga kura huku waangalizi wa kura wakitarajia idadi kubwa ya zaidi ya asilimia 80 kujitokeza kushiriki katika uchaguzi huu.
Serikali ya Uhispania hata hivyo imeimarisha usalama katika jimbo hilo ikihofia kuzuka vurugu.
Wizara ya ndani tayari imeshawapeleka maafisa wake wa usalama 15,000 kushika doria wakati huu wa uchaguzi, hii ikiwa ni kulingana na vyombo vya habari nchini humo.
Hata hivyo licha ya serikali ya Uhispania awali kujaribu kila mbinu ya kuzuwiya jimbo hilo kujitenga, wapiga kura wanasema bado azma yao iko pale pale.
Marc Botey mwanamuziki aliye na umri wa miaka 47 anasema ikiwa kiongozi mmoja ataondolewa mwengine atachukua nafasi yake, akisisitiza kuwa suala la kujitenga litaendelea bila kujali ni nani kiongozi wao.
Wakaazi bado waendelea na msimamo wao wa kutaka kujitenga
Kwa upande wake Antonio Hiborra mkaazi wa Catalonia anamatarajio ya uchaguzi wa leo kutoa fursa kwa jimbo hilo kujitenga.
"Tunatumai Jamhuri ya Catalonia itashinda. Hayo ni matumaini yangu kwasababu wakatolonia, sisi ambao ni asilimia 100 kwa 100 wakatalonia kwa miaka mingi tangu wakati wa wazazi wangu na babu zangu tumejihisi kama taifa. Tulijihisi tofauti kuliko wengine na ndio maana tunataka kuunda jamhuri yetu, na niaamini tutafika hapo hatimaye," alisema Antonia Hiborra.
Catalonia, jimbo tajiri kaskazini Mashariki mwa Uhispania lenye lugha na tamaduni tofauti na maeneo mengine Uhispania, hivi karibuni liliongozwa na serikali ya Carles Puigdemont aliyeongoza kura ya maoni ya kutaka kujitenga mnamo Oktoba mosi na kushinikiza mchakato wa kujitenga jimbo hilo na Uhispania.
Hatua hiyo ilisababisha mgogoro wa kikatiba ulioisukuma serikali ya kihafidhina mjini Madrid ya Waziri Mkuu wa Mariano Rajoy kuivunja kabisa serikali ya Catalonia na kuiweka chini ya usimamizi wa serikali kuu ya Uhispania, na kuitisha uchaguzi mpya wa majimbo mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Puigdemont na mawaziri wake wanne walikimbilia Brussels Ubelgiji huku wanachama wengine katika utawala wake wakizuiliwa na serikali hiyo ya Uhispania kwa madai ya kufanya uasi na matumizi mabaya ya fedha za umma kwa jukumu lake la kuongoza mchakato wa jimbo hilo kujitenga na Uhispania.
Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AFP/AP
Mhariri: Yusuf Saumu