1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yajadili mkopo wa tatu

10 Agosti 2015

Maafisa wa serikali ya Ugiriki wamejadili mswada wa makubaliano ya tatu ya kuiokoa nchi hiyo kiuchumi, ulioandikwa kwa misingi ya majadiliano na wakopeshaji wa Umoja wa Ulaya, na shirika la fedha la kimataifa IMF.

https://p.dw.com/p/1GCEj
Belgien Euro-Gipfel erzielt Einigung bei Griechenland
Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis TsiprasPicha: Reuters/E. Vidal

Afisa wa serikali ya Ugiriki amesema jana Jumamosi (08.08.2015), hali hiyo inaimarisha matumaini kwamba makubaliano yanaweza kufikiwa katika siku chache zijazo.

Ugiriki inaharakisha kufikia makubaliano ya kiasi cha euro bilioni 86 ifikapo mapema Jumanne, katika juhudi za kupata fungu la kwanza la msaada hapo Agosti 20. Wakati ambapo ikitakiwa kulipa deni kwa Benki Kuu ya Ulaya.

Griechenland Parlamentsabstimmung Sparauflagen
Bunge la Ugiriki linatarajiwa kuidhinisha makubaliano hayoPicha: Getty Images/AFP/L. Gouliamaki

Maafisa kutoka Umoja wa Ulaya na shirika la fedha la kimataifa IMF wamekutana na mawaziri wa fedha na uchumi mjini Athens jana Jumamosi (08.08.2015), siku moja baada ya maafisa wa fedha kufanya mkutano wao kwa simu na kudokeza kwamba kuna hatua zimepigwa katika mazungumzo hayo.

Mazungumzo hayo jana yalilenga katika kile kinachoelezwa kuwa ni, "hatua ya awali". Ugiriki inapaswa kupitisha kabla ya kukubaliwa kupatiwa mkopo, na pande hizo mbili zimefikia makubaliano kuhusu suala hilo, afisa mwandamizi wa serikali amesema bila ya kutoa maelezo zaidi.

Vikwazo bado vipo

Mazungumzo yataendelea leo Jumapili (09.08.2015) kujadili masuala mengine zaidi yanayoleta mvutano, afisa huyo amesema.

Deutschland Bundestag Sondersitzung Griechenland
Viongozi wa Umoja wa Ulaya walifanya mkutano maalum kuhusu UgirikiPicha: Reuters/A. Schmidt

"Makubaliano yatakamilishwa bila matatizo kabla ya Agosti 18, afisa huyo ameongeza.

Ugiriki imeepuka kwa tundu ya sindano kujitoa kutoka kanda ya sarafu ya euro mwezi uliopita baada ya miezi kadhaa ya majadiliano makali ambayo yamemalizika kwa waziri mkuu Alexis Tsipras kupata makubaliano ambayo yanaambatana na masharti magumu ya kubana matumizi na masharti ya mageuzi ili kuepuka nchi hiyo kuporomoka kiuchumi.

Majadiliano yaendelea vizuri

Tangu wakati huo majadiliano kuhusiana na makubaliano hayo, ambayo yatatoa maelezo kuhusu mageuzi na fedha zitakazotolewa -- yameendelea kwa hali nzuri, huku wakopeshaji wakiisifu Ugiriki kwa ushirikiano.

Mtazamo wa maafisa wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wa siku ya Ijumaa ni kwamba mazungumzo yanaendelea vizuri na huenda yakakamilika mwishoni mwa juma, chanzo kimoja kilichokaribu na suala hilo kimeeleza.

Symbolbild Griechenland EU Verhandlungen Schuldenkrise Fahne Flagge
Ishara ya Ugiriki na Umoja wa Ulaya kufanyamajadilianoPicha: Reuters/Y. Behrakis

Iwapo mswada wa makubaliano ya maelewano na tathmini iliyofanyiwa mabadiliko endelevu ya deni yatakuwa tayari kama ilivyopangwa siku ya Jumanne, serikali ya Ugiriki na bunge vitatarajiwa kuidhinisha mswada huo ifikapo Alhamis.

Hali hii itafungua njia kwa mawaziri wa fedha wa mataifa wanachama wa kanda ya sarafu ya euro kukutana ama wafanye mkutano kwa njia ya simu siku ya Ijumaa na kuidhinisha mpango wa mkopo huo utakaotolew kwa muda wa miaka mitatu kwa Ugiriki.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Yusra Buwahid