Serikali ya Tunisia yazungumzia kujiuzulu
24 Oktoba 2013Hotuba yake hiyo iliyotarajiwa kwa kiasi kikubwa anaitoa wakati kumetokea mapigano kati ya vikosi vya usalama na watu wenye silaha walioyazingira maeneo ya kati ya mkoa wa Sidi Bouzid nchini Tunisia. Mapigano hayo yamesababisha maafisa sita wa polisi kuuwawa ambapo vile vile waandamanaji wa upande wa upinzani walikusanyika katikati ya Tunis wakishinikiza kuondoka haraka madarakani kwa serikali yake.
Akizungumza baada ya kufanya mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri, Waziri Mkuu Larayedh alisema na hapa namnukuu" Leo hii tunarudia tena ile dhamira yetu ya kanuni ya kuachia madaraka kwa muongozo ulio katika mpango wa awamu tofauti. Na kuongoza jambo hilo halifanyiki kwa kumpendeza mtu bali kwa maslahi ya taifa.
Kauli nzito ya kisiasa
Kauli hiyo nzito katika siasa za Tunisia imetolewa jana wakati ambapo kumekuwepo na hamasa kubwa ya kusubiri mjadala wa kitaifa wa taifa hilo. Lakini hata hivyo Waziri Mkuu huyo amesema atajiuzulu tu baada ya katiba mpya ya taifa hilo kupitishwa.
Upande wa upinzani nchini humo umekuwa ukisubiri "kauli iliyo thabiti" kutoka kwa Larayedh ya kujiuzulu katika kipindi kisichozidi wiki tatu kama ilivyoanishwa na wapatanishi na kukubaliwa na chama chake cha Ennahda, kwa lengo la kutoa nafasi ya kuanza kwa mjadala wa kitaifa.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, mazungumzo lazima yafanyike kwa wiki tatu ili kuweza kuunda serikali mpya ya wataalamu. Wapatanishi watakuwa na mwezi mmoja kuweza kuidhinisha katiba, sheria za uchaguzi na ratiba ya kufanyika uchaguzi mpya. Hayo ni miongoni mwa vipengele muhimu ambavyo vimezuiwa kutokana na kuwepo kwa msuguano baina ya waislamu wenye itikadi kali, muungano wa washirika wao na upinzani.
Imani ya wasuruhishi
Hata hivyo wapatanishi wanaamini kwamba mazungumzo katika taifa hilo lililogawanyika kisiasa yatafanikisha hatua muhimu katika medani ya kisiasa na kuumaliza mgogoro ulioligubika taifa hilo tangu mwezi Julai mwaka huu, baada lile tukio la kuuwawa mbunge mmoja kutoka upande wa upinzani, Mohamed Brahimi, katika shambulio ambalo wanatuhumiwa wasilamu wenye msimamo mkali.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa mjadala wa kitaifa wa taifa hilo ulipaswa kuanza miaka miwili iliyopita baada ya Ennahad kuibuka kama chama kikubwa katika uchaguzi wa bunge la Tunisia, tukio ambalo lilifuatiwa na kuondolewa madarakani kiongozi mkongwe, Zine El Abidine Ben Ali. Makundi hayo ya Kiislamu yalionekana yenye kukandamizwa wakati wa uongozi wake.
Tangu uchaguzi huo, chama hicho kimekuwa kikinyong'onyeshwa na tuhuma za kutofanya jitihada za kutosha katika kulikwamua taifa kiuchumi, kuboresha maisha ya watu wake, vilevile kuonekana kama chachu za vurugu za kidini.
Mwandishi: Sudi Mnette AFPE
Mhariri:Josephat Charo