1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Somalia yatangaza mapambano

Halima Nyanza23 Machi 2011

Waziri mkuu wa Somalia ameahidi kulisaga kundi la wapiganaji wa al Shabaab katika kipindi cha miezi mitatu, wakati majeshi yake yanayoungwa mkono na vikosi vya jeshi la Umoja wa Afrika, yakidhibiti maeneo mapya.

https://p.dw.com/p/10g6g
Raia wamekuwa wahanga wa vita nchini SomaliaPicha: AP

Waziri mkuu wa Somalia, Mohamed Abdullahi Mohamed, ameiambia Radio ya serikali ya nchi hiyo kwamba majeshi ya nchi hiyo yamejiandaa vya kutosha kupambana na wapiganaji wa al-Shabaab, lakini hata hivyo haikufahamika wazi kwamba kauli yake hiyo inamaanisha kuanza kwa awamu ya pili ya mapambano makali kufanyika nchi nzima.

Waziri mkuu wa Somalia amesema vikosi vyao vimepiga hatua katika mapigano ya hivi karibuni na kundi la wapiganaji la Al Shabaab na kwamba ana matumaini kuwa watawaondoa na hatimaye kumaliza mzozo huo katika kipindi cha siku tisini, kuanzia jana.

Kamanda wa jeshi la Somalia, Jenerali Abdikarim Farah, amesema mashambulio yanaendelea  katika wilaya iliyo kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu, wakati majeshi ya serikali yakisonga mbele pia katika eneo lililokuwa likidhibitiwa na waasi kusini mwa Somalia.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa operesheni ya kijeshi inayofanywa mwezi huu dhidi ya kundi la al Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaeda inaweza kuwa ni hamasa za kisiasa, wakati viongozi wa nchi hiyo wakitaka kurejesha tena hadhi yao.

Wafadhili na mataifa yaliyo katika kanda hiyo, wiki chache zilizopita yalikosoa vikali mageuzi ya kisiasa na jinsi hatua zinavyokwenda polepole pamoja na kuimarika kwa hali ya usalama nchini humo, wakati ambapo serikali na bunge la mpito karibu kumaliza muda wake.

Kulingana na makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2009, serikali hiyo ya mpito ya somalia na bunge lake litamaliza muda wake Agosti 20 mwaka huu, na kwamba wakati huo wanapaswa kuanzisha katiba mpya na uchaguzi kufanyika.

Katika hatua nyingine Kenya imetuma wanajeshi wake katika mpaka wake na Somalia kuweza kuyasaidia majeshi ya nchi hiyo kupambana na waasi katika mji ulio mpakani wa Dobley.

Duru za usalama zimesema kuwa pia Kenya inaendelea kuimarisha nguvu katika eneo la mapambano ambako waakazi wake wanaripoti kuwepo kwa mapigano makali kati ya waasi, jeshi la Somalia na wanamgambo washirika wao.

Katika hatua nyingine msemaji wa serikali ya Kenya, Alfred Mutua, amekanusha taarifa kuwa majeshi ya nchi hiyo yameingia Somalia.

Amesema majeshi yao yamekuwa yakilinda mpaka wao, kutokana na kwamba hawataki Wasomali wavuke mpaka na kuingia Kenya na baadaye keleta mapigano yao nchini humo.

Awali chanzo cha habari kilisema kuwa  majeshi ya Kenya yameingia ndani ya Somalia kulisaidia jeshi la serekali nchi hiyo.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters

Mhariri: Miraji Othman