Serikali ya Somalia inaongeza vikwazo kudhibiti sekta ya habari
10 Oktoba 2007Vyombo vya habari vya nchini Somalia sasa vinahitajika kujiorodhesha upya katika wizara ya habari
Shirikisho la kimataifa la waandishi wa habari (IFJ) limelaani hatua hiyo ya serikali ya mpito ya Somalia ambayo linasema inalenga kukandamiza zaidi uhuru wa vyombo vya habari.
Amri hiyo mpya imetolewa na waziri wa habari wa Somalia Madobe Nurrow Mohammed imevitaka vyombo vya habari vya nchini humo vijiorodheshe katika ofisi za wizara ya habari.
Amri hiyo pia haikuvisalimu vyombo vya habari vya kimataifa ambavyo kuanzia sasa havitaruhusiwa kufanya kazi na vituo vya habari au kupokea ripoti kutoka kwa waandishi wa nchini Somalia kabla ya kupata kibali kutoka kwenye wizara ya habari.
Mkurugenzi wa shirikisho la kimataifa la waandishi habari IFJ kanda ya Afrika bwana Gabriel Baglo amesema katika taarifa yake kwamba shirikisho hilo la kimataifa limefadhaishwa mno na hatua iliyochukuliwa na waziri wa habari wa Somalia bwana Madobe Nurrow Mohammed.
Bwana Baglo ameitolea mwito serikali ya Somalia iyaache huru mashirika ya habari kufanya kazi na washirika wake bila ya kuingiliwa kati na serikali.
Waziri wa habari wa Somalia amekilaumu chama cha kitaifa cha waandishi wa habari nchini humo NUSOJ kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa katika kuorodhesha vitendo vya ukiukaji haki za upashaji habari.
Mkurugenzi huyo wa shirikisho la kimataifa la waandishi wa habari katika kanda ya Afrika Gabriel Baglo amesema kwenye taarifa yake iliyopokelewa mjini Nairobi, Kenya kwamba juhudi za waandishi wa habari wa nchini Somalia zinapaswa kuungwa mkono.
Makundi ya kutetea haki za binadamu yametowa mwito wa kulindwa waandishi wa Somalia.
Mwaka huu waandishi wa habari saba waliuwawa.
Vilevile katika hali isiyo eleweka vyema waandishi habari kadhaa wamekamatwa na kutiwa kizuizini.
Hivi majuzi tu vyombo vya habari vilifichua juu ya waandishi wa habari watano wa Somalia waliotekwa nyara na kuibiwa mali zao.
Somalia ni nchi ya pili duniani ambayo usalama wa waandishi wa habari unatishiwa ikifuatia Irak.
Taifa hilo la upembe wa Afrika halijakuwa na serikali kamili tangu kiongozi wa nchi hiyo Mohamed Siad Barre alipong’olewa kutoka madarakani mwaka 1991.