1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Nigeria yayapuuza matakwa ya Boko Haram

Admin.WagnerD15 Mei 2014

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan amepuuzilia mbali uwezekano wa kuwaachia huru wapiganaji wa kundi la waasi wa Boko Haram kama sharti la kuwaachia wasichana wa shule waliotekwa nyara mwezi mmoja uliopita na kundi hilo

https://p.dw.com/p/1C0VU
Picha: Reuters

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika Mark Simmonds ambaye yuko nchini Nigeria kwa mazungumzo kuhusu operesheni ya kuwaachia huru wasichana hao zaidi ya mia mbili waliotekwa nyara kutoka shuleni mwao amewaambia wanahabari kuwa Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ameweka bayana kuwa hakutakuwa na mazungumzo kati ya serikali yake na Boko Haram yatakayojumuisha suala la kuachiwa kwa wapiganaji wa kundi hilo wanaozuiwa na serikali kama mojawapo ya matakwa ya kuwaachia wasichana hao.

Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau alioenekana katika mkanda wa video Jumatatu wiki hii akisema yuko tayari kuwaachia wasichana hao iwapo wapiganaji wake walioko magerezani wataachiwa.

Waziri wa mambo ya ndani wa Nigeria Abba Moro alipinga mara moja pendekezo hilo na kusema kundi la waasi haliwezi kuweka masharti ya kipi kifanywe na serikali.

Mengine yazungumzwe ila si kuachiwa kwa wapiganaji

Hata hivyo serikali ya Nigeria imesema iko tayari kujadili na kundi hilo la waasi wenye itikadi kali kuhusu masuala mengine kama maridhiano ili kumaliza uasi hasa kaskazini mwa nchi hiyo.

Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau
Kiongozi wa Boko Haram Abubakar ShekauPicha: picture alliance/AP Photo

Kutupiliwa mbali kwa uwezekano huo wa kuachiwa kwa wafungwa ili wasichana hao wa shule waachiwe huru kunakuja huku juhudi za jumuiya ya kimataifa kuisadia Nigeria kuwatafuta na kuwaokoa wasichana hao zikipamba moto.

Marekani imeshaanza operesheni za kutumia ndege za kijeshi zisizotumia marubani na zinazoendeshwa na marubani kufanya uchunguzi wa kutambua walipo wasichana hao.

Hata hivyo Marekani imetangaza kuwa bado haijaanza kutoa taarifa za kijasusi kuhusu operesheni zao kwa jeshi la Nigeria kutokana na kwamba bado hakuna makubaliano rasmi ya kiitifaki kuhusiana na usalama wa taarifa hizo.

Juhudi za kimataifa zapamba moto

Uingereza, Ufaransa, Israel na China pia zinahusika katika shughuli hizo za uokozi zinazolenga eneo la kaskazini mwa Nigeria hasa katika msitu wa Sambisa licha ya kuibuka hofu kuwa huenda baadhi ya wasichana hao wamesafirishwa hadi nchi jirani au kugawanywa katika makundi.

Baadhi ya wasichana waliotekwa nyara na Boko Haram
Baadhi ya wasichana waliotekwa nyara na Boko HaramPicha: picture alliance/abaca

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema viongozi wa nchi za Benin, Cameroon, Niger na Chad watakutana na Jonathan mjini Paris Jumamosi hii katika mkutano wa kilele wa usalama ambao pia utahudhuriwa na wawakilishi kutoka umoja wa Ulaya, Uingereza na Marekani.

Mkutano huo utajadili jinsi ya kulitokomeza kundi la Boko Haram na kutoa mafunzo kwa majeshi ya kanda hiyo katika kukabiliana na makundi ya waasi huku rais Jonathan akitafuta idhini ya bunge kuongeza muda wa hali ya hatari kwa miezi sita katika majimbo matatu ambayo ni ngome ya Boko Haram Borno, Yobe na Adamawa.

Huku hayo yakijiri kiasi ya wanajeshi wanne na wapiganaji kadhaa wa Boko Haram wameuana katika mji wa Maiduguri katika kisa cha kufyatuliana risasi badaa ya waasi hao kuwashambulia wanajeshi hao walipokuwa wakisafiri.

Tukio hilo lilizua ghadhabu miongoni mwa wanajeshi hao zilizoelekezwa kwa kiongozi wao ambaye aliwaamuru kupitia eneo hilo licha ya hapo awali kuelezea wasiwasi wao kuwa si salama kusafiri usiku kutokana na uwezekano wa kushambuliwa na Boko Haram.

Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Josephat Charo