1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya muungano wa vyama vikuu magazetini

16 Desemba 2013

Mada moja tu imehodhi vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani hii leo:Serikali kuu ya muungano kati ya vyama vya Christian Democratic Union CDU,Christian Social Union CSU na wana Social Democratic wa SPD.

https://p.dw.com/p/1AaGi
Große Koalition Vertragsunterzeichnung
Picha: Reuters

Maoni ya wahariri yanatofautiana kuhusu hata hivyo kimoja wanakubaliana:SPD licha ya kupoteza kura katika uchaguzi mkuu wa septemba 22 iliyopita hakijaondoka patupu katika wezani wa madaraka serikalini.

Tunaanzia na Rhein Zeitung linalotathmini mhula huu wa tatu wa kansela Angela Merkel madarakani.Gazeti linaandika:Kansela Angela Merkel anaanza mhula wa tatu mgumu madarakani. Matokeo ya uchaguzi ya asili mia 41.5 hakuyatumia ipasavyo katika mkataba wa serikali ya muungano.Muungano huu wa pili pamoja na wana Social Democratic ni wa bahati nasibu. Kwa sababu SPD imejitwika jukumu,kwa kuitisha kura ya maoni ya wafuasi wake, la kutekeleza kile wanachokitaka,la sivyo hawatochelea kusababisha kuvunjika serikali kuu.

Gazeti la "Hamburger Abendblatt linaandika:Mshindi mkubwa wa serikali ya muungano wa vyama vikuu ni mwenyekiti wa chama cha Social Democratic Sigmar Gabriel aliyejitosa katika bahari ya hatari ya kuwauliza wanachama maoni yao na kushinda.Zoezi hilo ndio chanzo cha kupata ridhaa kubwa kutoka kwa Angela Merkel na wakati huo huo kupata ridhaa ya walio wengi pia chamani.Wana Social Democratic wanaonyesha kupata nguvu kuliko wakati wowote ule mwengine katika kipindi cha miaka hii ya karibuni

Wezani wa Nguvu kati ya Vyama Ndugu

Gazeti la "Kieler Nachrichten "linachambua wezani wa nguvu katika serikali kuu mpya ya muungano.Gazeti linaandika:"Baraza jipya la mawaziri litakaloongozwa na kansela Angela Merkel linaleta wezani mpya wa kugawana madaraka miongoni mwa vyama ndugu vya Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union CSU. Ni kichekesho kuona hapo awali jinsi mwenyekiti wa chama cha CSU Horst Seehofer alivyokuwa akijaribu kuzitembeza wizara za usafiri, kilimo na misaada ya maendeleo kama ushindi kwa jimbo lake la Bavaria.Lakini ukweli haufichiki,hata maneno yawe matamu vipi!Nyadhifa muhimu hivi sasa zinashikiliwa na chama ndugu cha CDU.Kwa hivyo ushindi mkubwa katika uchaguzi wa jimbo la Bavaria haukusaidia kitu. Na ushindi mkubwa zaidi wa kansela ,bila ya shaka ni uamuzi wake wa kumchagua von der Leyen kuwa waziri wa ulinzi. Si jukumu rahisi kwa bibi huyo mwenye umri wa miaka 55. Lakini akifanikiwa kuleta mageuzi katika jeshi la shirikisho basi atakuwa anainyemelea ile nafasi anayoimezea mate ya kumrithi siku moja kansela Angela Merkel.

SPD Sigmar Gabriel präsentiert SPD Minister Kabinett Nahles 15.12.2013
Mwenyekiti wa chama cha SPD akitangaza majina ya mawaziri wa chama chakePicha: Reuters

Nyota mbili Serikalini

Hata gazeti la Hannoversche Allgemeine lina maoni sawa na hayo,linapoandika: Mwanamke kukabidhiwa wizara ya ulinzi,tovuti zilijaa habari mwishoni mwa wiki na kuna wale ambao hawakutaka au hawakuweza kuamini.Lakini walitulia na kutafakari,wametambua hii ni fursa ya aina pekee kuwa na mtu kutoka nje kulifanyia marekebisho jeshi la shirikisho. Von der Leyen atabidi adhihirishe anaweza.Na akiweza,basi atajizidishia sifa katika daraja ya kimataifa,mbali na Sigmar Gabriel wa SPD,na CDU pia itakuwa imempata nyota kwa jina la Ursula von der Leyen.

Ursula von der Leyen Porträt Politikerin
Waziri mpya wa ulinzi Ursula von der LeyenPicha: JOHANNES EISELE/AFP/Getty Images

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef