Serikali ya Muungano kuundwa Uturuki
8 Juni 2015Naibu Waziri Mkuu Numan Kurtulmus amesema anaamini Waziri Mkuu anaweza kuunda serikali ya muungano ndani ya muda aliyopangiwa kufanya hivyo. Chama tawala kina takriban siku 45 za kuunda serikali hiyo au uchaguzi wa haraka ufanyike iwapo kitashindwa kufanya hivyo.
Aidha Chama cha rais Recep Tayyip Erdogan cha AKP kilishinda asilimia 41 ya kura zilizopigwa hapo jana na kilitabiriwa kuchukua viti 258 vya bunge ikiwa ni upungufu wa viti kumi nane kuiwezesha kuunda serikali peke yake.
Ushindi huu umekatiza tamaa ya Erdogan ya kutanua madaraka yake katika mfumo mpya wa urais nchini humo.
Aidha Waziri Mkuu Ahmet Davutoglu alitarajiwa kuitisha mkutano na baraza lake la mawaziri na wakuu wa chama chake hii leo ili kujadili mustakabal wa chama hicho wakati utawala wake wa miaka 13 ukielekea ukingoni.
Matokeo hayo ya uchaguzi pia yamesimamisha matumaini ya Erdogan ya kubadilisha katiba ili kumpa madaraka makubwa zaidi uongozini.
Wakati huo huo vyama vyote vitatu vya upinzani vimejitokeza dhidi ya hatua ya kuunda serikali ya muungano na chama tawala cha AKP hii ni baada Erdogan kuongoza kampeni kali ya kukipigia debe chama chake bila kuzingatia matakwa ya katiba ya nchi hiyo.
Hata hivyo upinzani umesema uchaguzi huu umeonesha namna uturuki ilivyokuwa kisiasa na namna watu wan chi hiyo wanavyozingatia demkotrasia ya kweli.
Upinzani wagoma kufanya kazi na chama tawala cha AKP
Uturuki inasiku 45 za kuunda serikali ya Muungano. Lakini chama cha wa kurdi cha HDP kimesema hakiko tayari kuwepo katika muungano huo.
"Tumewaahidi watu wetu kwamba hatutaunda muungano wa ndani au wa nje na chama tawala cha AKP," alisema kiongozi wa chama hicho, Selahattin Demirtas.
Kwa upande mwengine chama kikuu cha upinzani nchini humo cha CHP, kimependekeza kupewa jukumu hilo la kuunda serikali ya muungano, huku chama cha wazalendo cha MHP kinachoongozwa na Devlet Bahceli kikionesha kusita kufanya kazi na chama tawala na kupendekeza kufanyika kwa uchaguzi wa haraka.
Mwandishi: Amina Abubakar Reuters/AP/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu