1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya mjini Tripoli yasema Misri imetangaza vita

22 Juni 2020

Serikali ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa jana ililaani onyo lililotolewa na Misri la kuingia kijeshi nchini Libya. Serikali hiyo imelitaja tangazo hilo la Misri kuwa ni kutangaza vita. 

https://p.dw.com/p/3e9hd
Ägypten Kairo 2019 | Abdel Fattah al-Sisi, Präsident & Chalifa Haftar
Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/H. Presidency of Egypt

Mjini Tripoli serikali inayotambuliwa kimataifa ilitowa taarifa siku ya Jumapili ikisema kitendo cha Misri ni cha uchokozi na cha uingiliaji wa moja kwa moja wa masuala ya Libya na ni tangazo la vita.

Makabiliano ya maneno kati ya pande hizo mbili yamekuja katika siku ya mkesha wa mkutano wa video wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa nchi za kiarabu kuhusu Libya ambapo serikali hiyo ya GNA ilikataa kushiriki mkutano huo.

Siku ya Jumamosi rais wa Misri Abdel Fatah al Sisi alitowa onyo kwamba ikiwa wanajeshi wa serikali ya mjini Tripoli watasogea hadi kwenye mji wa Sirte ambao ni mji muhimu wa kimkakati ulioko kiasi kilomita 450 kutoka mashariki mwa Tripoli basi huenda wakaifanya Misri iingilie kati moja kwa moja .

Al-Sisisi droht mit Militäreinsatz in Libyen Interventionsbedrohung Kriegserklärung
Waandamanaji wakiwa na picha ya kumpinga rais Abdel-Fattah Al-Sisi wa MisriPicha: picture-alliance/AA/H. Turkia

Lakini kwa upanse wa serikali hiyo ya Libya uingiliaji kati wa masuala ya ndani ya nchi yake,kushambuliwa kwa uhuru wa mamlaka yake iwe ni kwa kutolewa matamshi kama yaliyotolewa na rais wa Misri au kwa kuwaunga mkono wanaotaka kufanya mapinduzi,wanamgambo na mamluki yuko ni mambo yasiyokubalika.

Serikali hiyo ya Libya kwa hivyo imeitaka jumuiya ya Kimataifa kuchukua majukumu yake kuhusiana na suala hilo la kuongezeka mgogoro. Inasema kwamba milango yake iko wazi kwa mazungumzo ya uwazi yasiyoegemea upande chini ya muongozo wa Umoja wa Mataifa lakini haikubali katu juhudi za upande mmoja au zisizozingatia sheria.

Kumbuka Libya iko kwenye mapambano ya kuwania madaraka kati ya pande mbili hasimu toka mwaka 2015,upande mmoja ukiwa ni serikali iliyoweka makao yake mjini Tripoli na ambayo inatambuliwa na Umoja wa Mataifa na upande wa pili uliojitangazia uhalali wa kuiongoza Libya ukiwa mashariki mwa nchi hiyo ambako ndiko kwenye bunge lililochaguliwa, chini ya kamanda mwenye sauti Khalifa Haftar.

Libya nchi yenye utajiri wa mafuta iko kwenye vita vikubwa vinavyohusisha wanamgambo waliogawika kwa misingi ya kikabila,makundi ya siasa kali na mamluki tangu mwaka 2011 alipoondolewa madarakani na kuuwawa aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Moamer Kadhafi-kupitia harakati zilizoungwa mkono na nchi za Magharibi hususan Jumuiya ya kujihami ya NATO.

Libyen-Ägypten-Waffenruhe
Hawa ni wapiganaji tiifu kwa serikali ya inayotambulika kimataifaPicha: Getty Images/AFP/M. Turkia

Hivi sasa juhudi za serikali ya GNA kusogea mbele kwenye vita zimekwama nje ya mji wa pwani wa Sirte mji ambao ni muhimu kabisa wa visima vya mafuta ambao uko chini ya udhibiti wa Haftar na majeshi yake. Kutokana na juhudi za serikali ya mjini Tripoli za kutaka kuutwaa mji huo kutoka mikononi mwa Haftar,ndipo Misri ilipoingia na rais Al Sisi kutoa onyo Jumamosi kupitia televisheni akisema mji huo wa Sirte na Al Jufra kuelekea kusini ni eneo la mstari mwekundu na katu Misri haitokaa kuitazama serikali hiyo ya Libya kutwaa eneo hilo ambako Misri inasema inahitaji kulinda mpaka wake.

Serikali ya GNA kwa upande wake ikatoa jibu kwa kuiambia Misri kwamba Libya nzima ni mstari mwekundu na kwa maana haitoruhusu wananchi wake wachokozwe au kutishiwa.

Saumu Yusuf