Serikali ya Libya yakanusha kuwa inasaidiwa na Uturuki
29 Desemba 2019Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki ametahadharisha kwamba mgogoro wa nchini Libya unaweza kutumbukia katika vurumai na kwamba nchi hiyo inaweza kugeuka Syria nyingine. Waziri huyo Mevlut Cavusoglu amesema hayo wakati akifanya juhudi kwa lengo la kupitisha sheria ya kuiwezesha Uturuki kupeleka majeshi nchini Libya.
Serikali ya Libya inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa imekuwa inakabiliana na majeshi ya jenerali muasi Khalifa Haftar yanayoungwa mkono na Urusi,Misri,Umoja wa Falme za Kiarabu na Jordan.
Waziri Cavusoglu amesema ikiwa Libya itageuka kuwa Syria nyingine na nchi zote za kanda zitaathirika. Waziri huyo alisema hayo alipokuwa anahutubia kwenye mkutano wa chama tawala nchini Uturuki AKP. Amesema inapasa kufanya kila linalopasa kuepusha vurumai na kugawaynika kwa Libya. Ameeleza kuwa hicho ndicho hasa kinachofanywa na nchi yake Uturuki. Ametamka kuwa Uturuki inashirikiana na serikali halali ya nchini Libya.
Majeshi ya jenerali muasi Haftar mpaka sasa bado hayajaweza kuingia mjini Tripoli lakini taarifa zinasema vikosi vyake vimepata mafanikio ya kiasi fulani kusini mwa mji huo kutokana na msaada wa wapiganaji kutoka Urusi na Sudan. Kwa mujibu wa taarifa za kidiplomasia ndege zisizokuwa na rubani za Umoja wa Falme za Kiarabu zimesaidia.
Ndege hizo zimemwezesha jenerali Haftar kudhibiti vita vya angani kwa sababu ndege hizo zinadondosha mabomu mara nane zaidi kulinganisha na ndege zinazotumiwa na serikali halali ya Libya zinazotoka Uturuki. Mwezi uliopita Uturuki na serikali ya Libya GNA zilitiliana saini mkataba wa ushirikiano katika masuala ya kijeshi na usalama na mkataba mwingine juu ya ulinzi wa miapaka ya baharini.
Wakati huo huo serikali ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa imekanusha madai kwamba waasi wa Syria wanaoungwa mkono na Uturuki wanapigana bega kwa bega na wanajeshi wa serikali hiyo. Tamko la kukanuhsa madai hayo limetolewa baada ya kinachodaiwa kuwa mkanda wa video uliowaonyesha waasi hao wakizungumza lahaja ya kiarabu cha Syria.
Siku ya Jumamosi shirika linalofuatilia masuala ya haki za binadamu nchini Syria lilidai kwamba waasi wa Syria wapatao 300 wanaoshiriiana na Uturukli waliwasili nchini Libya. Shirika hilo limesema wapiganaji hao wamekusanyika kwenye kambi ya serikali ya Libya kwenye sehemu hatari ya kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli. Hata hivyo jeshi la Syria linalojiita la kitaifa linaloungwa mkono na Uturuki limekanusha madai hayo.
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Cavusoglu anatarajiwa kukutana na vingozi wa upinzani siku ya Jumatatu na serikali ya Uturuki inatazamiwa kujadili mswaada juu ya kupeleka majeshi nchini Libya.
Wiki iliyopita Rais Erdogan alifahamisha juu ya uamuzi wa serikali yake kuhusu kupata ridhaa ya bunge juu ya kupeleka majeshi ya Uturuki nchini Libya ili kuilinda serikali ya nchi hiyo inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa ambayo inakabiliwa na kitisho cha vikosi vya jenerali muasi Khalifa Haftar. Hatua hiyo imesababisha hofu, huenda mgogoro wa Libya ukatifua mgogoro wa kikanda.
Wakati huo huo Spika wa Bunge la Libya ameitaka jumuiya ya kimataifa ipinge uhalali wa serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ambayo inashirikiana na Uturuki.
Vyanzo: (RTRE/DPA)