Bolivia yawasilisha bungeni mapendekezo ya uchaguzi mpya
21 Novemba 2019Akazungumza na waandishi habari mjini La Paz, rais Anez amesema ana matumaini kuwa mapendekezo ya serikali yatawezesha kufanyika uchaguzi mkuu haraka iwezekanavyo na kuleta mwafaka wa kitaifa.
Wabunge wanatarajiwa kuanza kujadili mapendekezo hayo yanayolenga pia kuutangaza uchaguzi uliofanyika Oktoba 20 kuwa batili baada ya kuandamwa na madai ya kuweko wizi wa kura.
Anez amesema mapendekezo aliyowasilisha yatawezesha kuundwa kwa tume mpya ya uchaguzi na itatokana na maridhiano kati ya makundi ya raia nchini Bolivia. .
Waziri wa sheria wa Bolivia Alvaro Coimbra amesema ni matuamini ya walio wengi kwamba bunge litaidhinisha haraka muswada huo ili kuruhusu kuundwa kwa tume mpya ya uchaguzi itakayopanga tarehe ya uchaguzi mwingine.
Chama cha Morales chawasilisha mapendekezo yake
Chama cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Evo Morales, cha MAS pia kimetuma bungeni mapendekezo kama hayo ya kutaka kuandaliwa uchaguzi mwingine.
Jumuiya ya mataifa ya eneo la Amerika ambayo iligundua kasoro kadhaa katika uchaguzi uliopita nchini Bolivia, imeunga mkono pendekezo la serikali na kutoa wito wa kuitishwa haraka kwa uchaguzi mwingine nchini humo.
Pendekezo hilo la serikali limekuja baada ya watu kadhaa kuuwawa Jumanne usiku kwenye makabiliano na vikosi vya usalama katika kituo kimoja cha mafuta kwenye mji mkuu La Paz.
Aliyekuwa rais wa nchi hiyo Evo Morales, amevituhumu vikosi vya usalama vya Bolivia kwa kuendesha mauaji ya halaiki dhidi ya wafuasi wake na ametaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua.
Kwa wiki kadhaa wafuasi wa Morales wamekuwa wakizifunga barabara muhimu kutoka mikoa inayoongoza kwa kilimo hali iliyosababisha upungufu wa chakula na nishati ya mafuta kwenye mji mku La Paz na miji mingine.
Kwanini Bolivia imo kwenye mkwamo?
Machafuko yalizuka nchini Bolivia baada ya Morales, rais wa kwanza kutoka jamii za wazawa wa nchi hiyo, kutuhumiwa kuiba kura ili kubakia madarakani katika uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita,.
Kiongozi huyo alijiuzulu na kukimbilia Mexicobaada ya kupoteza uungwaji mkono wa vikosi vya usalama.
Tangu kujiuzulu kwake wafuasi wake wamekuwa wakifanya maandamano kwenye mitaa ya mji mkuu na majimbo mengine kumtaka rais wa mpito aondoke madarakani.
Hapo jana serikali ya Bolivia ilitoa mkanda wa sauti ya mtu anayedhaniwa kuwa Morales ikiamuuru wanachama wa vuuguvugu la upinzani kuendelea kuweka vizuizi barabarani kote nchini humo.
Jumuiya kadhaa za kimataifa, zikiwemo Umoja wa mataifa, Umoja wa Ulaya na Kanisa Katoliki zimekuwa zikijaribu kutafuta nafasi ya kufanyika mazungumzo kati ya serikali ya mpito na vyama vya upinzani vinavyomuunga mkono Morales lakini hata hivyo hakuna mafanikio yaliyopatikana.