1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Assad yazidi kulaumiwa

MjahidA3 Mei 2013

Kundi la Upinzani nchini Syria limesema kwamba utawala wa rais Bashar Al Assad ndio uliohusika katika mashambulio dhidi ya kijiji cha wasunni na kusababisha mauaji ya watu 50.

https://p.dw.com/p/18RAo
Bashar Assad
Bashar AssadPicha: picture alliance / AP Photo

Kulingana na mkuu wa shirika la kutetea haki za binaadamu lililo na makao yake makuu jijini London Rami Abdel Rahman, vikosi vya Syria vilivyoungwa mkono na wapiganaji waliotiifu kwa serikali hiyo waliingia katika kijiji cha Bayda hapo jana na kufanya Mashambulizi. Shirika hilo limesema huenda watu zaidi ya 100 wakawa wameuwawa katika mashambulizi hayo.

Hii leo muungano wa kitaifa nchini Syria umeishutumu serikali ya Assad kufanya mauaji hayo huku ukisema kuwa wanawake na watoto ni miongoni mwa waliouwawa na watu wengi mpaka sasa bado hawajulikani waliko.

Waasi Syria
Waasi SyriaPicha: Miguel Medina/AFP/Getty Images

Sasa kundi hilo limeitaka Jumuiya ya nchi za kiarabu pamoja na Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka ili kuwanusuru wakaazi wa kijiji cha Bayda.

Shirika la kutetea haki za binaadamu limesema watu katika kijiji hicho walidungwa visu, na kupigwa risasi.

Hata hivyo Umoja wa Mataifa umesema watu takriban 70,000 wameuwawa nchini Syria tangu kuanza kwa mapigano nchini humo miaka miwili iliopita.

Marekani yafikiria kuwahami waasi Syria

Huku hayo yakiripotiwa, Marekani imesema inaangalia upya uwezekano wa kuwapa silaha waasi wa Syria kufuatia ukandamizaji zaidi unaofanywa dhidi yao na vikosi vya serikali.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amesema baada ya rais Barack Obama kukataa hapo awali hatua ya kuwapa waasi silaha sasa wanaangalia upya uwezekano wa kuwahami waasi hao.

Akiwa ziarani nchini Mexico Obama alisema kwamba kutokana na umwagikaji mwingi wa damu nchini Syria, na matumizi ya silaha za sumu hii imewalazimisha kuangalia kila uwezekano wa kuwalinda raia.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck HagelPicha: REUTERS

Kwa upande wake waziri wa ulinzi Chuck Hagel amesema kwa sasa hakuna hatua yoyoyte ilioafikiwa huku akikataa kutoa maoni yake binafsi juu ya swala hilo.

Brahimi kujiondoa katika juhudi za amani

Hata hivyo juhudi za kumaliza mzozo wa Syria huenda zikaingia doa kutokana na mpatanishi mkuu wa mzozo huo Lakhdar Brahimi kuonekana kutaka kujiondoa katika wadhifa wake huo.

Wanadiplomasia wanasema kwamba wanachama wote wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa yani Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani wote wangelipenda Brahimi aendelee na jukumu lake la kuongoza juhudi za kutafuta amani nchini Syria.

Mpatanishi wa mzozo wa Syria Lakhdar Brahimi
Mpatanishi wa mzozo wa Syria Lakhdar BrahimiPicha: Reuters

Kulingana na mwanadiplomasia mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina,Brahimi tayari ameshaamua kuwa anajiondoa katika wadhifa huo kwa hivyo wanachosubiri ni uamuzi huo kutangazwa rasmi .

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman