'Serikali Nigeria imeshindwa kuizuwia Boko Haram'
30 Septemba 2013Makamo huyo wa zamani wa rais wa Nigeria Atiku Abubakar amesema katika taarifa iliyonukuliwa na gazeti la Vanguard la leo Jumatatu, kuwa ipo haja ya kuangalia upya mkakati wa nchi hiyo, wa kukabiliana na kundi hilo aliloliita la 'waoga.' Abubakar alisema anasononeshwa na mauaji ya wanafunzi waliokuwa wamelala katika bweni katika mji wa Gubja, jimboni Yobe mwishoni mwa wiki.
Mashuhuda wa tukio hilo, waliliambia shirika la habari Uingereza Reuters, kuwa wapiganaji, ambao wanashukiwa kuwa wanachama wa kundi la Boko Haram, walilivamia bweni hilo, na kuwapeleka baadhi ya wanafunzi nje kabla ya kuwaua, na wengine walipigwa risasi wakati wakijaribu kutoroka.
Kundi hilo ambalo linataka kuanzisha utawala wa sheria za Kiislamu kaskazini mwa Nigeria, limezidisha mashambulizi dhidi ya raia katika wiki za hivi karibuni, katika kile kinachosemekana ni kulipiza kisasi, dhidi ya mashambulizi ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya ngome zao.
Shule zalengwa zaidi
Shule kadhaa, ambazo zinaonekana kama fokasi ya mfumo wa elimu na utamaduni wa kimagharibi, zimekuwa zikilengwa zaidi na mashambulizi hayo. Makamo wa rais wa zamani Atiku Abubakari alisema kuwa raia wa Nigeria sasa wamepoteza imani na serikali yao kutokana na kukosa dira katika kushughulikia masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya taifa hilo.
Rais Goodluck Jonathan alilielezea shambulizi hilo kuwa ni la kishetani, na kusema kuwa wakati umefika kubadilisha mbinu za kukabiliana na waasi hao.
"Nilipotangaza hali ya hatari mashambulizi yalipungua, lakini sasa baada ya muda wanaanza kuangalia maeneo rahisi, ambako mtu hawezi kuwataraji kama vile mabweni ya wanafunzi, ilimradi tu waifedheheshe serikali.
Sasa wakati umefika kubadili mbinu, maana ngoma ikibadilika, mchezaji pia anabadilika. Kwa hiyo tunawahakikishia Wanigeria kuwa tutaendelea kufanya kile kilichosahihi kwa nchi hii, bila kuhatarisha maslahi ya raia wa kawaida," alisema rais Jonathan.
Kiticho kinachoongezeka
Kundi la Boko Haram na makundi mengine ya Kiislamu kama Ansaru yaliyo na mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda, yamegeuka kuwa kitisho kikubwa zaidi kwa usalama wa taifa la Nigeria, iliyo na uchumi wa pili kwa ukubwa barani Afrika, na muuzaji mkubwa wa mafuta.
Serikali za mataifa ya magharibi nazo zinazidi kuwa na wasiwasi juu ya kuongezeka kwa makundi kama hayo, kuanzia nchini Mali na Algeria katika Sahara, hadi Kenya mashariki mwa Afrika, ambako wapiganaji wa kundi la Kisomali la Al-Shabaab waliwaua watu wasiopungua 67 katika shambulio dhidi ya kituo cha biashara mjini Nairobi wiki moja iliyopita.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre, dpae,
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman