Serikali na waasi wakubaliana Jamhuri ya Afrika ya Kati
20 Juni 2017Makubaliano hayo yaliyosimamiwa na kundi la amani la Saint Egidio kutoka Kanisa Katoliki katika makao yake makuu mjini Roma, yanataka mapigano yasitishwe mara moja na pia yanatoa wito wa kutambuliwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais uliopita.
Makubaliano hayo yaliyojadiliwa katika kipindi cha siku tano, yamesifiwa na kutajwa kama fursa ya kuiimarisha mojawapo ya nchi maskini na zenye machafuko zaidi duniani. Chini ya makubaliano hayo, makundi yaliyojihami yatawakilishwa katika uwanja wa kisiasa na badala yake mashambulizi yasitishwe na wanachama wake watajumuishwa katika jeshi la nchi hiyo.
Jamhuri ya Afrika ya Kati imekumbwa na mapigano ya kidini na kikabila tangu mwaka 2013, pale waasi wa Seleka ambao wengi ni Waislamu walipochukua mamlaka, jambo lililowafanya waasi wa anti-Balaka ambao wengi ni Wakristo kuanza mapigano.
Makubaliano hayo yatashuhudia kufunguliwa njia zote za mawasiliano
Kundi la Sant Egidio ambalo lilikuwa mpatanishi katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Msumbiji mwaka 1992, limekuwa likijaribu kutafuta amani katika Jamhuri hiyo ya Afrika ya Kati kwa miezi kadhaa. Marco Impagliazzo ni rais wa kundi hilo.
"Leo tumetia saini makubaliano yaliyo na changamoto kubwa kwa pande zote, pamoja na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na uongozi wake," alisema Marco, "ili kusitishwa kwa mapigano kuafikiwe, na kufunguliwe pia njia zote za mawasiliano ili hatimaye kuwe na uhuru nchini humo."
Makundi ya waasi yaliahidi kuhakikisha kuna uhuru wa watu kutembea na bidhaa kusambazwa, kwa kuondoa vizuzi kama hatua ya kwanza inayotokana na makubaliano hayo. Pande zote pia zilikubaliana kurejesha mamlaka kwa uongozi wa taifa kote nchini humo. Charles Armel Doubane ni waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliyehudhuria kutiwa saini kwa makubaliano hayo.
Kuna wengine hawaamini iwapo makubaliano hayo yataheshimiwa
"Kwetu sisi haya yamekuwa makubaliano muhimu kwa uwiano nchini mwetu na kwa amani ya baadae katika Jamhuri ya Afrika ya Kati," alisema Armel. "Kwasababu hiyo niko hapa kuiambia jamii ya Sant Egidio, serikali ya Italia na jamii ya kimataifa kwamba, tuliweka juhudi kuhakikisha tunaitimiza ndoto yetu ya pamoja, ambayo ni ndoto ya kuwa na nchi yenye amani."
Lakini wengine wana ati ati kuhusiana na makubaliano hayo. Philipe Barga mwenye umri wa miaka 40 mjini Bangui, alisema viongozi wa waasi hawakushikilia mikataba waliyotia saini hapo awali. Nikiyanukuu maneno yake,amesema "ni wale wanaotia saini mikataba hiyo wasiyoiheshimu, siyaamini makubaliano haya," mwisho wa kunukuu.
Mizozo ya kisiasa imeikumba nchi hiyo mara kwa mara na mapigano ya kulipiza kisasi yanaongezeka kwa mara nyengine licha ya uchaguzi wa mwaka jana uliolenga kumaliza umwagikaji damu.
Katika kipindi cha wiki mbili mwezi Mei, mapigano kati ya makundi ya waasi yalipelekea vifo vya watu 300 na kuwaacha wengine 100,000 bila makaazi.
Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu