Serikali mpya ya Ujerumani
Kufuatia Chama cha Social Democrat (SPD) kuridhia muungano mkuu na wahafidhina wa Christian Democrats (CDU/CSU), pande hizo mbili zimetangaza watu watakaochukuwa nafasi za uwaziri mukiwa na baadhi ya sura za kushangaza.
Muhula wa tatu wa Merkel
Kile kilichokuwa tayari kiko wazi baada ya uchaguzi mkuu wa shirikisho sasa ni cha uhakika: Angela Merkel ataendelea kuwa kansela wa Ujerumani kwa muhula mwengine, akiongoza muungano mkuu unaoundwa na Christian Democratic Union (CDU), chama dada cha Bavaria CSU na Social Democrat (SPD). Muungano kama huo ulikuwa madarakani kutoka mwaka 2009 hadi 2009, wakati wa muhula wa kwanza wa Merkel.
Waziri ‘mkubwa’
Mwenyekiti wa SPD, Sigmar Gabriel, amepachikwa la “waziri mkubwa” na vyombo vya habari vya Ujerumani. Sasa ataongoza wizara mpya ya uchumi na nishati, itakayosimamia mkakati wa kitaifa kutoka nishati ya nyuklia kwenda nishati jadidifu. Gabriel ana uwezekano mkubwa pia wa kuwa naibu kansela.
Arudi mambo ya nje
Nafasi ya waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani itajazwa na Frank-Walter Steinmeier, mwenyekiti wa zamani wa wabunge wa SPD. Aliwahi kushikilia uwaziri huo wakati wa muhula wa kwanza wa Angela Merkel (2005 hadi 2009) na kuwa naibu kansela kutoka 2007 hadi 2009. Alipigania ukansela mwaka 2009 lakini akashindwa na Merkel.
Ang’ang’ania Fedha
Nafasi ya waziri wa fedha inaonekana kuendelea kuwa mikononi mwa Wolfgang Schäuble wa CDU. Akiwa na miaka 71, Schäuble ndiye waziri mkongwe kabisa na aliyehudumu muda mrefu zaidi serikalini. Alikuwa mkuu wa ofisi ya kansela wakati wa Kansela Helmut Kohl mwaka 1984. Amekuwa akitembelea kiti kiti cha magurudumu tangu aliponusurika jaribio la kumuua mwaka 1990.
Mwanamikakati mzoefu
Kijana wa Merkel asiyeyumba: Thomas de Maizière anachukuliwa kama mwepesi wa kubadilika na muungaji mkono wa kutegemewa wa kansela. Baada ya kukabiliana na ukosoaji akiwa waziri wa ulinzi, sasa anarudi kwenye nafasi ya waziri wa mambo ya ndani, ambayo mwanasheria huyo aliishikilia kuanzia mwaka 2009 hadi 2011.
Waziri wa kwanza mwanamke wa ulinzi
Tayari ilishafahamika kuwa Ursula von der Leyen angelikuwa kwenye baraza jipya, lakini habari kwamba waziri huyo wa zamani wa kazi atakuja kuwa waziri wa ulinzi zilikuwa za kushangaza. Kazi hii inaonekana kuwa nguvu kwa mama huyu wa watoto saba. Mageuzi ya kimsingi kwenye jeshi yanaendelea, na matumizi ya wizara hiyo yamekosolewa katika siku za karibuni.
Himaya ya ajira kwa Nahles
Andrea Nahles atakuwa waziri wa kazi na masuala ya kijamii. Hadi sasa, ni katibu mkuu wa chama cha SPD na anafahamika kwa kujinasibisha na kundi la mrengo wa shoto la chama hicho. Hivi karibuni alilichangamsha bunge kwa kunakili na kuimba nyimbo ya watoto wakati wa hotuba ya kuikosoa serikali.
Ghafla kaonekana
Moja ya walioshangaza kwenye baraza jipya ni Heiko Maas wa SPD, ambaye atakuwa waziri wa sheria na ulinzi wa walaji. Maas amekuwa mwanasiasa asiyefahamika. Mwaka 2004 na 2009 alishindwa na mgombea wa CDU katika nafasi ya waziri mkuu wa jimbo la Saarland. Amekuwa mjumbe wa kamati kuu ya SPD tangu 2001.
Uso wa kijana wa SPD
Hata kabla ya SPD kutangaza mawaziri wake, ilishafahamika sana kwamba Manuela Schwesig angelijaza nafasi ya waziri wa masuala ya familia, wazee, wanawake na vijana. Akiwa na umri wa miaka 39, ni mjumbe kijana kabisa kwenye baraza la mawaziri. Hadi sasa amehudumu kama waziri wa kazi, usawa wa kijinsia na masuala ya kijamii katika serikali ya jimbo la Mecklenburg-Western Pomerania.
Kutoka mweka hazina hadi waziri
Barbara Hendricks alikuwa akifanya kazi nyuma ya pazia akiwa mweka hazina mkuu wa SPD. Kwa nafasi yake mpya ya waziri wa mazingira, atakuwa kwenye jukwaa la wazi la kisiasa. Hata hivyo, sekta ya nishati haitakuwa chini ya wizara yake, kwani sasa kuna wizara mpya ya uchumi na nishani inayoongozwa na Sigmar Gabriel.
Kada wa chama
Kutoka meneja wa kampeni wa Angela Merkel hadi waziri wa afya, katibu mkuu huyu wa zamani wa CD ametunukiwa wadhifa huo. Herrmann Gröhe anajua namna ya kuendesha kampeni. Bila ya shaka atapaswa kufanya kazi kidogo kwani hadi sasa hajawahi kufahamika kuwa mtaalamu wa mambo ya afya.
Mshirika muhimu wa Merkel
Ingawa bado haijawa rasmi, mkuu mpya wa afisi ya kansela na hivyo mmoja wa watu wa karibu sana na kansela atakuwa Peter Altmaier wa CDU, ambaye hadi sasa ndiye waziri wa mazingira. Akiwa mkuu wa afisi ya kansela, atakuwa pia na dhima ya kuratibu kazi za shirika la ujasusi la Ujerumani, akichukua nafasi ya Ronald Pofalla.
‘Waziri wa Intaneti’ anayejiamini
Alexander Dobrindt wa CDU hafahamiki kuwa na heshima – akiwa katibu mkuu wa zamani wa chama, alimuita Sigmar Gabriel “mtu mnene na mwenye kipaji cha chini”. Wawili hao sasa watafanya kazi pamoja katika baraza la mawaziri, ambapo Dobrindt anachukua uongozi wa idara ya miundombinu ya dijiti. Wizara hiyo inasimamia usafirishaji wa data za Ujerumani ili kuhakikisha kuwa zinaweza kubeba maendeleo.
Profesa aongoza wizara ya elimu
Wizara ya elimu pia itashuhudia muendelezo ambapo Johanna Wanka ataendelea kuwa mkuu wake. Aliichukua wizara hiyo mwezi Februari 2013 baada ya mtangulizi wake, Annette Schavan, alipojiuzulu kwa tuhuma za kudanganya maandiko. Wanka, ambaye ni mtaalamu wa hisabati, alikuwa mhadhiri kwenye Chuo Kikuu cha Sayansi cha Merseburg.
Mhafidhina mwenye utata
Wengine wanaweza kuchukulia ni kushushwa cheo kwa waziri wa zamani wa mambo ya ndani Hans-Peter Friedrich, ambaye atasimamia usambazaji chakula na kilimo. Friedrich alikosolewa kwa namna alivyoishughulikia kashfa ya ujasusi ya NSA, lakini mwanasiasa na mwanasheria huyu wa CDU hatashuka jukwaani akiwa kiongozi wa wizara ya kilimo.
Uso mpya wa CSU
Gerd Müller atakuwa mkuu mpya wa wizara ya maendeleo. Akiwa waziri wa zamani wa kilimo, ataendelea kuyafanyia kazi masuala ya maendeleo ya kilimo na ushirika. Lakini hili litakuwa jukumu lake kwa umma mjini Berlin.
Waziri wa kwanza mwenye asili ya Kituruki
Aydan Özoguz, binti wa wahamiaji wa Kituruki, sasa atakuwa waziri mpya wa uhamiaji, wakimbizi na ujumuishaji wageni. Mwanamke huyo wa miaka 46 kutokea Hamburg amekuwa mbunge tangu mwaka 2009, na alichaguliwa kuwa naibu mkuu wa SPD mwaka 2011. Anachukuwa wizara hii kutoka kwa Maria Böhmer wa CDU.
Mwanasiasa wa Utamaduni mwenye uzoefu
Mwanasiasa wa CDU, Monika Grütters, ni waziri mpya wa utamaduni. Ana dhamana ya taasisi na miradi muhimu ya kitamaduni na “uwakilishi wa kitamaduni wa taifa zima”. Mwanahistoria huyu ya sanaa ana mahusiano mazuri sana na Kansela Merkel. Mtangulizi wake, Bern Neumann, hatakuwamo tena serikalini.