1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali mpya ya Libya yaanza kazi

3 Juni 2014

Serikali mpya ya Libya imetangaza kuwa imeanza kufanya kazi, licha ya hatua ya waziri mkuu anayeondoka Abdullah al-Thani kukataa kuwachia madaraka. Hayo yanajiri wakati machafuko yakiendelea mashariki mwa nchi.

https://p.dw.com/p/1CAzH
Libyen Premierminister Ahmed Maiteeq
Picha: Reuters

Waziri Mkuu, Ahmed Maiteeq, mwenye umri wa miaka 42, amesema katika taarifa yake kuwa aliandaa kikao cha baraza lake la mawaziri kwa mara ya kwanza tangu aliposhinda uchaguzi wa mwezi Mei, wakati kukiwa na mgogoro wa kugombea madaraka nchini humo. aidha amesema

Msemaji wa waziri huyo mkuu amesema hakukuwa na matatizo yoyote kuingia katika jengo la bunge. Maiteeq ndiye waziri mkuu wa tano wa Libya tangu Muamar Gaddafi alipoondolewa madarakani na kuuawa katika vuguvugu la umma mwaka wa 2011.

Bunge lilimchagua mfanyabiashara Maiteeq anayeungwa mkono na wafuasi wa itikadi za Kiislamu katika uchaguzi uliojaa vurugu mapema mwezi Mei, siku chache baada ya watu wenye silaha kulivamia bunge ili kuvuruga shughuli ya upigaji kura.

Hata hivyo, baadhi ya wapinzani wa kisiasa wamekataa kumkubali kiongozi huyo. Maiteeq anatarajiwa kuongoza kwa kipindi kifupi cha mpito hadi pale uchaguzi wa bunge utakapofanyika mnamo Juni 25, na kisha bunge jipya kuchukua usukani na kuunda baraza jipya la mawaziri.

Libyen Kämpfe in Bengasi Universitätsgebäude beschädigt
Jeshi la Jenerali Mstaafu Khalifa Haftar linapambana na wanamgambo wenye msimamo mkali mjini BenghaziPicha: picture-alliance/dpa

Wakati huo huo, mapigano makali baina ya wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu na wanajeshi watiifu kwa Jenerali Mstaafu, Khalifa Haftar, katika mji wa mashariki wa Benghazi yalisababisha vifo vya watu 21 hapo jana. Maafisa wa hospitali katika mji huo wa bandari wamesema karibu wanajeshi 11 ni miongoni mwa waliouawa na watu 112 wamejeruhiwa. Waziri Mkuu Maiteeq alilaani machafuko hayo baina ya wapiganaji wanaodaiwa kuwa wa kundi la Ansar al-Sharia na wanajeshi.

Serikali ya waziri mkuu anayeondoka al-Thani imesema inaandaa “mkutano wa dharura” kuhusiana na machafuko hayo, ambayo wakaazi wanasema yamepungua. Hayo ndiyo machafuko makubwa zaidi kushuhudiwa tangu watu 76 walipouawa katikati ya mwezi Mei wakati Jenerali Haftar alipoanzisha mashambulizi aliyoyaita kuwa ni “Operesheni ya kurejesha heshima” ili kuyaangamiza makundi yenye itikadi kali za Kiislamu nchini Libya anayoyaita kuwa ni ya “kigaidi”.

Kundi la al-Qaida tawi la Maghreb limewataka Walibya kupambana na Haftar na Jeshi lake la Kitaifa, likimtaja kuwa ni “adui wa Uislamu”. Maafisa nchini humo wanampinga Haftar wakisema ni mhalifu asiyelindwa na sheria, lakini baada ya maelfu ya Walibya kumuunga mkono anasema ana jukumu kutoka kwa watu kuuangamiza “ugaidi”. Maafisa wa serikali ya mpito, wanaokabiliwa na mgogoro wa kugombania madaraka, hawajaweza kusitisha machafuko wakiwa hawana jeshi wala polisi imara.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef