Waziri wa mambo ya nje wa Urusi ziarani nchini Burundi
30 Mei 2023Lavrov ambaye amepokelewa na mwenzake wa Burundi Albert Shingiro, amesema uhusiano kati ya nchi hizi mbili umekuwa ukiimarika na ndio sababu idadi ya wanafunzi wa burundi wanao kwenda kusoma chuo kikuu Urusi imeongezwa kutoka 50 hadi 100 katika mwaka 2023 kuelekea 2024.
Katika mahojiano na waandishi habari baada tu ya kukutana kwa mazungumzo na mwenzi wake wa Burundi, Albert Singiro, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Serguei Lavrov amesema uhusiano kati ya Burundi na nchi hiyo umekuwa ukiimarika na kwamba mwezi julay kutafanyika mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika na Urusi, na itawakilishwa kwenye ngazi ya juu.
Isitoshi Urusi imekuwa ikiisaidia Burundi katika Sekta za Afya na Elimu, na tayari idadi ya wanafunzi wanao kwenda kusomea Urusi kwa ngazi ya chuo kikuu imeongezeka kutoka wanafunzi 50 hadi 100 katika mwaka wa masomo wa 2023 kuelekea 2024. Na kwamba tayari kimezinduliwa kwenye chuo kikuu cha Burundi kituo cha kusomesha wanafunzi lugha ya kirusi.
Waziri Serguei Lavrov amesema wamezungumzia pia mswala ya kikanda na kimataifa, na kwamba kuna umuhimu wa kuwepo na demokrasia inapo hitajika kunzumzia uonevu aloutajwa kuendeshwa na nchi za magharibi.
" Tunaridhishwa kuona tuna msimamo mmoja katika maswala mengi ya kimataifa, na tumezungumzia umuhimu wa kuwepo na uheshimishaji wa sheria za Umoja wa mataifa, hususan inapohusika Uhuru wa nchi, hii ni sheria inayokiukwa mara kwa mara na Marekani na washirika wake."
Serguei Lavrov amesema pia wamezungumzia umuhimu wa kulifanyia marekebisho baraza la usalama la Umoja wa mataifana kwamba bara la Afrika, vile vile Asia na Amerika Kusini yapate uwakilishi wa kudumu. Kuhusiana na vita vya Ukraine waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Urusi amekumbusha sababu zilopeleka vita hivyo huku akikaribisha msimamo wa Burundi.
Hata hivyo mwenyeji wake Albert Shingiro amesema Burundi ilichukuwa msimamo wa kutoegemea upande wowote katika vita hivyo, kwa kuwa wapo upande wa kutafuta jawabu na kuepusha vita kuziathiri nchi nyingine.
" Kuhusu vita vya Ukraine, Burundi ilichukuwa uamuzi wa kutoegemea upande wowote, na kuwa upande wa kutafuta jawabu kwa vita hivyo na huo ndio msimamo wa nchi nyingi za Afrika juu ya swala hilo."
Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Urusi anatarajiwa kukutana kwa mazungumzo na rais Evariste Ndayishimiye jioni hii atakapo kuwa karejea nchini akitokea Nigeria.