Serbia na harakati za kutaka kuingia Umoja wa Ulaya
25 Oktoba 2010Serbia imefanikiwa kukiondoa kizingiti kikubwa kilichokuwa kimesalia katika harakati zake za kutaka uwanachama katika Umoja wa Ulaya. Hii leo Umoja huo umekubaliana kuitathmini nafasi ya Serbia kama mgombea wa kutaka kujiunga na jumuiya hiyo. Uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya umekuja baada ya Serbia kulegeza msimamo wake kuelekea jimbo la Kosovo.
Makubaliano yaliyofikiwa na Umoja wa Ulaya juu ya Serbia yanaitaka nchi hiyo kuimarisha ushirikiano wake na mahakama ya kimataifa juu ya Uhalifu ya ICTY pamoja na kufufua juhudi zake za kutaka kuwafikisha mbele ya sheria wahalifu sugu wa kivita wa eneo hilo la Balkans kama vile Ratko Mladic.
Akizungumzia kuhusu uamuzi wa Umoja wa Ulaya juu ya kuiruhusu Serbia kugombea kujiunga na Umoja huo, Uamuzi ambao umefikiwa baada ya wiki kadhaa za mivutano, waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji, Steven Vanackere, amesema ni hatua ya mwanzo kwa Serbia katika kujiunga na Umoja huo wenye wanachama 27.
Ubelgiji ambayo kwa sasa inashikilia wadhifa wa kupokezana wa mwenyekiti wa Umoja huo wa Ulaya imeonya, hata hivyo, kwamba hatua ya kuikubalia kabisa nchi hiyo kujiunga na chombo hicho bado ipo mbali, huku Belgrade ikiendelea kutiwa kishindo kusafisha hadhi yake. Waziri Steven amesema ni lazima ieleweke wazi kwamba Serbia bado inahitajika kuchukua hatua zaidi hatua mpya ambazo zitazingatia masharti kuhusu kushirikiana kikamilifu na mahakama ya ICTY.
Aidha makubaliano ya Umoja huo yametoa mwito kwa halmashauri ya Umoja huo kutoa mtazamo wake juu ya pendekezo la Belgrade la kutaka kugombea uwanachama katika Umoja huo, hatua ambayo ni muhimu kabisa katika mchakato wa kuwania kuwa mgombea wa uwanachama katika Umoja huo wa Ulaya.
Upande mwingine, mawaziri hao wa Umoja wa Ulaya pia wamekubaliana kwamba ikiwa Serbia Itasaidia kufanikisha kukamatwa kwa Mladic na Goran Hadzic wanaosakwa na mahakama ya ICTY, basi itadhihirisha kwamba inataka ushirikiano wa dhati na mahakama hiyo siku za usoni.
Belgrade imeridhika na uamuzi uliofikiwa wa kusogezwa mbele pendekezo lake la kutaka kugombea kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya. Waziri wa Ulinzi wa Serbia, Dragan Sutanovac, amesema safari ya nchi hiyo kuelekea katika Umoja wa Ulaya haisimami.
Mwandishi Saumu Mwasimba/DPAE AFPE
Mhariri Othman Miraji.