1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sera za Kilimo za Umoja wa Ulaya kufanyiwa marekebisho

P.Martin20 Mei 2008

Leo hii Kamisheni ya Umoja wa Ulaya katika mkutano wa Bunge la Ulaya mjini Strasbourg,inapendekeza mpango wa kufanya mageuzi katika sera za kilimo za umoja huo.

https://p.dw.com/p/E2yv

Azma ni kupunguza malipo ya ruzuku kwa wakulima na wakati huo huo kuongeza uzalishaji wa vyakula ili kutimiza mahitaji yanayoendelea kuongezeka.

Mawaziri wa Kilimo wa Umoja wa Ulaya walikutana siku ya Jumatatu mjini Brussels kutayarisha mapendekezo hayo ya mageuzi.Miongoni mwa mageuzi yanayopendekezwa ni kufutilia mbali mfumo wa kulipa ruzuku kwa wakulima wanaozalisha bidhaa zisizohitajiwa sana na vile vile hatua kwa hatua kuondosha viwango vya uzalishaji wa maziwa.

Mawaziri hao wa kilimo,walikubaliana kuwa ipo haja ya kuchukua hatua zitakazosaidia kudhibiti bei za vyakula barani Ulaya na kuongeza uzalishaji wa vyakula.Lakini hawakuweza kukubaliana vipi sera za kilimo za Umoja wa Ulaya,zifanyiwe mageuzi huku hali inayokutikana hivi sasa ikitiwa maanani.

Suala la kupunguza ruzuku ya kilimo,lilipingwa na wengi wao,lakini Uingereza imeshikilia kuondosha malipo hayo.Waziri wa Kilimo wa Uingereza Hilary Benn amesema,"litakuwa kosa kubwa kuendelea kuwalipa wakulima wa Ulaya ruzuku,kwani kwa kufanya hivyo nchi zinazoendelea zitazidi kuwa na shida kuongeza mazao yao kilimo na kuuza bidhaa hizo katika masoko ya Umoja wa Ulaya." Amesema,duniani kuna chakula cha kutosha - tatizo la watu katika nchi zinazoendelea ni bei za vyakula.

Wakati huo huo,Waziri wa Kilimo wa Slovenia IZTOK JARC alieongoza mkutano wa Brussels amesema, zichukuliwe hatua zitakazoweza kutuliza masoko.Kwa maoni yake bei za vyakula si tatizo pekee - kuna tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa na ongezeko la bei ya mafuta pia.

Kwa upande mwingine,Kamishna wa Kilimo wa Umoja wa Ulaya,Mariann Fischer Boel amesema,ni muhimu kwa Ulaya kuendelea kuongeza mazao yake ya kilimo,lakini bila ya kuathiri mazingira.Kwa maoni yake,pesa zitakazopatikana kwa kupunguza au kuondosha malipo ya ruzuku,zitumiwe kuhifadhi mazingira na kuchangamsha miradi ya ajira katika sehemu za mashambani.Kamishna huyo hasa anatazamia kupunguza ruzuku zinazolipwa kwa makampuni makubwa ya kilimo,ambayo kila mwaka hupokea zaidi ya Euro 100,000.

Hivi sasa tayari wakulima wanaopokea ruzuku ya zaidi ya Euro 5,000 hupunguziwa malipo hayo kila mwaka kwa asilimia 5.Sasa Kamishna wa Kilimo anataka kupunguza ruzuku hiyo hatua kwa hatua hadi kiwango cha asilimia 13 ifikapo mwaka 2012.Na makampuni makubwa ya kilimo ndio yanatazamiwa kupunguziwa zaidi yaani,hadi asilimia 22.Kamisheni ya mjini Brussels inasema,mpango huo ni marekebisho ya kuboresha sera za kilimo za Umoja wa Ulaya.