1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia yakosolewa kwa kuweka sera kali ya kigeni

13 Agosti 2018

Saudi Arabia linataka kuweka sera kali ya kigeni ili kuwakabili wakosoaji. Wachambuzi wanasema huenda mgogoro na Canada kuhusu mashambulizi ya anga nchini Yemen huenda ukasababisha kuwapo shinikizo zaidi la kimataifa.

https://p.dw.com/p/335LN
Saudi-Arabien | Kronprinz Mohammad bin Salman
Mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin SalmanPicha: picture-alliance/AA/Saudi Kingdom Council/B. Algaloud

Itakumbukwa shambulio la angani lilitekelezwa na Muungano wa kijeshi unaoongozwa na  Saudi Arabia katika eneo la Kaskazini mwa Yemen Alhamisi wiki iliyopita, na kuwaua watu arubaini na tatu waliokuwamo kwenye basi, wengi wakiwa watoto wa shule, huku Marekani na Umoja wa Ulaya yakitaka uchunguzi kufanywa kuhusiana na kisa hicho.

Muungano huo ulisisitiza kwamba waasi wa Houthi walikuwamo kwenye basi hilo, lakini mashirika ya habari ya kimataifa yalichapisha picha za watoto wakikimbizwa hospitalini, huku wakilazimika kuvumilia mgogoro ambao umekuwa ukishuhudiwa kwa miaka mitatu. Umoja wa Mataifa umeutaja mgogoro huo kuwa mbaya zaidi wa kibindamu kuwahi kutokea kote duniani.

Mmoja wa wachambuzi wa eneo la Mashariki ya Kati  anayeishi jijini Washington Marekani, Sigurd Neubauer, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, nikimnukuu, ‘' Vita hivyo vinaendelea kukosa maana katika jamii ya kimataifa likiwamo kongamano la Marekani. Shambulio hilo kwa bahati mbaya limekuwa desturi wala si la ubaguzi'' mwisho wa kumnukuu.

Shambulio hilo la bomu, ambalo ni mojawapo ya mwingilio unaoashiria msimamo dhabiti wa Mfalme Mohammed Salman wa Saudi Arabia kuhusu sera hiyo ya kigeni, linafuatia mzozo wa kidiplomasia na Canada mapema wiki hii. Saudi Arabia ilimfurusha balozi wa Canada nchini humo na kumrejesha balozi wake kutoka Canada, vile vile kusitisha biashara na uwekezaji baada ya mji wa Ottawa kutangaza hadharani kwamba wanataka wanaharakati wa haki za kibinadamu waliozuiliwa nchini humo waachiliwe huru.

Saudi arabia iliwaondoa mamia ya wanafunzi kutoka vyuo vikuu nchini Canada, huku Shirika la Ndege la falme hiyo likisitisha safari zake kuelekea Toronto na  vile vile kusitisha huduma za kimatibabu nchini humo.

Saudi Arabia yawadhibiti wakosoaji wake

Hatua hiyo imeonekana kuashiria jinsi taifa la Saudi Arabia lenye utajiri mkubwa wa mafuta lisivyokuwa  tayari kukosolewa, katika masuala ya kigeni au ya nchi hiyo. Baadhi ya wachambuzi wanasema uongozi wa serikali ya nchi hauna wasiwasi kuhusu athari zinazoweza kutokana na hatua walizochukua dhidi ya Canada.

Belgien Nato-Gipfel
Justin Trudeau ambaye ni Waziri Mkuu wa CanadaPicha: Reuters/R. Krause

Hata hivyo Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, amekataa kurejea nyuma na kusema kwamba nchi yake itaendelea kuzungumzia haki za kibinadamu.'' Tunaendelea kujihusisha katika masuala ya kidiplomasia na kisiasa na Saudi Arabia. Tunaheshimu umuhimu wao katika masuala mbalimbali na kutambua kwamba wamepiga hatua katika baadhi ya masuala muhimu. Hata hivyo tutaendelea kutoa mchango wetu kuhusu haki za kibinadamu hapa kwetu na katika mataifa mengine kila kunapokuwa na haja ya kufanya hivyo.''

Kwa upande wake Msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani Heather Nauert amesema wamelizungumzia suala la Canada na serikali ya Saudi Arabia, na kusema kwamba pande zote mbili zinafaa kusuluhisha suala hilo kwa pamoja kidiplomasia. '' Tunazishauri serikali zote mbili kusuluhisha masuala yanayowahusu kwa pamoja. Hilo ni jambo ambalo sisi hatuwezi kulifanya, lazima tulitatue kwa pamoja. Ni suala la kidiplomasia na Saudi Arabia na Canada wanaweya kulitatua.''

Kwa sasa inaarifiwa kwamba Canada inatafuta ushauri wa mataifa ya Ujerumani na Sweden , ambayo awali yalishambuliwa na Saudi Arabia kwa  kuikosoa  kuhusu  ukiukaji wake wa  haki za kibinadamu. Vile vile inapanga kutafuta ushauri kutoka kwa mataifa mengine ya kiarabu  na Uingereza ambayo yamekuwa na ushirikiano thabiti wa kihistoria na Saudi Arabia.

Wakati huo huo Canada imeghadhabishwa na viongozi wa mataifa ya Magharibi ikiwamo Marekani ambayo ilitoa silaha za mabilioni ya pesa kwa muungano huo unaoongozwa na  Saudi Arabia , kwa kushindwa kuiunga mkono Canada .

Mwandishi: Sophia Chinyezi

Mhariri: Mohammed Abulrahman