Seoul.Bibi Condoleezza Rice awasili Seoul.
19 Oktoba 2006Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Bibi Condoleezza Rice amewasili mji mkuu wa Korea ya Kusini, Seoul ikiwa ni kituo chake cha pili katika safari yake ya mataifa manne ya bara la Asia.
Lengo la safari yake hiyo ni kuitia kishindo Korea ya Kaskazini kufuatia jaribio lake la bomu la nyuklia.
Kufuatia mazungumzo aliyoyafanya Bibi Condoleezza Rice nchini Japan na waziri mwenziwe wa mambo ya kigeni Taro Aso, bibi Rice ameionya Pyongyang dhidi ya nia yake ya kufanya jaribio la pili la nyuklia.
Safari ya bibi Rice nchini Japan, Korea ya kusini, China na Urusi ina nia ya kutafuta kuungwa mkono na mataifa hayo juu ya kuiwekea vikwazo Korea ya Kaskazini.
Akielezea mafanikio yake katika ziara yake nchini Japan, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Bibi Condoleezza Rice amesema.
“Waziri wa mambo ya kigeni na mimi, tumeahidiana kushirikiana na pamoja na mataifa mengine ili kuharakisha utekelezaji na kufanya utekelezaji huo uwe wa manufaa katika mambo yote yaliyokubaliwa katika azimio nambari 1718“.
Korea ya Kaskazini imeviita vikwazo hivyo kuwa ni “Tangazo la vita“ na kusema kwamba itapambana na nchi yoyote inayounga mkono vikwazo hivyo.