SEOUL: Ufyatulianaji wa risasi watokea katika mpaka wa Korea Kaskazini na Korea Kusini
1 Agosti 2006Matangazo
Wanajeshi wa Korea Kaskazini na Korea Kusini wamefyatuliana risasi katika eneo la mpaka wao uliojengewa ukuta, kwa mara ya kwanza katika kipindi cha mwaka mmoja.
Afisa wa jeshi amesema wanajeshi wa Korea Kaskazini walifyatua risasi mara mbili kwa kituo cha usalama cha Korea Kusini karibu na eneo lisilokaliwa tena na wanajeshi hii leo. Wanajeshi wa Korea Kusini nao wakafyatua risasi mara sita lakini hakuna aliyejeruhiwa katika tukio hilo.
Taarifa iliyotolewa na wakuu wa majeshi ya nchi hizo inasema tume ya Umoja wa Mataifa inachunguza kisa hicho.
Wakati huo huo, Korea Kaskazini imefutilia mbali sherehe ya pamoja na Korea Kusini iliyokuwa imepangwa ifanyike tarehe 15 mwezi huu katika mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang.