1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SEOUL : Marekani yazidi kuishinikiza Korea Kaskazini

20 Machi 2005
https://p.dw.com/p/CFV3

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice ameionya Korea Kaskazini kwamba kususia kwake mazungumzo ya nuklea hakuwezi kuendelea milele.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Seoul Rice amesema suala hilo linahitaji kutatuliwa pia amefuta uwezekano wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya serikali mbili ya Washington na Pyongyang na kusema kwamba mawasiliano kati ya nchi hizo yanaweza kufanyika tu wakati wa mazungumzo ya nchi sita juu ya suala hiyo yanayozijumuisha Marekani yenyewe, China, Russia, Japani na Korea zote mbili ile ya Kaskazini na Kusini.

Rice hivi sasa yuko nchini China ambapo amekutana na Rais Hu Jintao wa China leo hii na kuzungumzia suala tata la Taiwan pamoja na mazungumzo ya nuklea ya Korea Kaskazini.

Rais Hu amekaririwa akisema kufuatia mkutano wake na Rice kwamba ziara yake itakuwa na manufaa kwa China na Marekani kuimarisha baadhi ya masauala yanayozihusu nchi hizo kwa pamoja na pia itaendeleza uhusiano wa tija kati ya nchi hizo.

China ni kituo cha mwisho cha ziara ya Rice kwa mataifa sita ya Asia.