1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Seoul. Korea yakubali kushiriki katika mkutano wa nchi sita.

26 Julai 2005
https://p.dw.com/p/CEqe

Nchi sita zinazojaribu kutafuta suluhisho la mzozo juu ya mpango wa Korea ya kaskazini wa silaha za kinuklia zimekutana katika duru ya nne ya mazungumzo hayo mjini Beijing leo Jumanne baada ya miezi 13 ya mkwamo.

Mjumbe wa Korea ya kaskazini katika mazungumzo hayo ya nchi sita amesema leo kuwa suala kuu ni kulifanya eneo la rasi ya Korea kutokuwa na silaha za kinuklia , na kusisitiza kuwa ujumbe wake uko tayari kufanyakazi kuelekea katika lengo hilo.

Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Korea ya kaskazini Kim Kye Gwan amesema katika ufunguzi wa kikao hicho , kuwa kazi hiyo inahitaji msimamo thabiti wa kisiasa na mkakati wa uamuzi wa pande zote zinazohusika na ambazo zina nia thabiti ya kumaliza kitisho cha vita vya kinuklia.

Taarifa ya Bwana Kim katika mkutano huo iliyotangazwa moja kwa moja katika televisheni ya China , haikujumuisha mapendekezo mapya ama masharti mapya juu ya kuanza kwa mkutano huo.

Mapema mwaka 2005 Korea ya kaskazini ilijitangaza kuwa ni taifa lenye silaha za kinuklia.