SEOUL: Korea Kusini yakaribisha uamuzi wa Korea Kaskazini kumaliza mpango wake wa nyuklia
3 Septemba 2007Korea Kusini imeikaribisha hatua ya Korea Kaskazini kukubali kumaliza mpango wake wa nyuklia kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Hata hivyo mjumbe wa Korea Kusini katika mazungumzo ya mataifa sita, Chun Yung Woo, ameonya kwamba mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika katika pande sita huenda yakawa magumu.
Mjumbe huyo ameyasema hayo siku moja baada ya mpatanishi mkuu wa Marekani katika mzozo wa nyuklia wa Korea Kaskazini, Christopher Hill, kutangaza kwamba Korea Kaskazini imekubali kumaliza mpango wake wa nyuklia katika mkutano uliofanyika mwishoni mwa juma mjini Geneva nchini Uswisi.
´Nadhani hii ni muhimu na bila shaka tutatakiwa kuratibu vipengele katika mazungumzo ya mataifa sita. Kama nilivyokuwa nikisisitiza mara nyingi, mchakato huu sio kati ya pande mbili bali pande sita. Lakini tumefikia makubaliano mazuri kwamba tunatakiwa kuongeza kasi na tuimalize awamu hii mwaka huu wa 2007.´
Hill amesema kwa mara ya kwanza Korea Kaskazini imeweka tarehe ya kuumaliza mpango wake wa nyuklia tangu makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa mjini Beijing mnamo mwezi Februari mwaka huu, ambapo serikali ya Pyongyang ilikubali kukifunga kinu cha nyuklia cha Yongbyon.