1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SEOUL: Korea Kusini yaanza juhudi za kuwakoa mateka wake

26 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBey

Korea Kusini imeanza juhudi za kidiplomasia kuwaoka mateka wake 22 wanaozuiliwa na watekaji nyara nchini Afghanistan. Mjumbe wa Korea Kusini, Baek Jong - Chun, ameondoka leo mjini Seoul kwenda Afghanistan.

Baek Jong Chun ni katibu mkuu anayehusika na sera za kigeni na usalama katika ofisi ya rais na amekwenda Afghanistan kama mjumbe maalumu wa rais wa Korea Kusini Roh Moo - Hyun.

Ziara yake inafanyika kufuatia kuuwawa kwa mateka mmoja miongoni mwa mateka 23 waliotekwa nyara na wanamgambo wa Taliban.

Korea Kusini imelaani vikali kuuwawa kwa mchungaji wa kanisa la Kiprotestanti la Presbiteri mjini Seoul, Bae Hyung-Kyu, aliyekuwa akiwaongoza wenzake kufanya mradi uliodhaminiwa na kanisa hilo nchini Afghanistan.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais wa Korea Kusini, Roh Moo Hyun, imesema mauaji ya raia asiye na hatia ni kitendo kiovu ambacho hakiwezi kuhalalishwa kwa sababu yoyote ile na wala hakiwezi kuvumilika.

Msemaji wa Taliban, Qari Mohammed Yousuf, amesema leo mateka wote 22 wako salama kufuatia ahadi waliyopewa na serikali kwamba suluhisho la amani litapatikana kuhusiana na swala hilo.