1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Seneti yadai ushahidi wa Flynn kuhusu Urusi

11 Mei 2017

Kamati ya masuala ya ujasusi katika Baraza la Seneti imetoa hati ya kumtaka aliyekuwa mshauri wa usalama wa Trump Michael Flynn kuwasilisha nyaraka zinazohusiana na uchunguzi wa Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani

https://p.dw.com/p/2cmN6
USA Michael Flynn in Washington
Picha: picture-alliance/abaca/R. Sachs

Hayo ni wakati hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump kumtimua Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi la Marekani – FBI James Comey imeonekana kuwagawa Wamarekani kwa misingi ya kisiasa na kuutumbukiza utawala wake katika msukosuko. 

Mwenyekiti wa chama cha Republican Seneta Richard Burr na naibu mwenyekiti wa chama cha Democratic katika kamati hiyo Seneta Mark Warner, wametoa taarifa ya pamoja wakisema jopo hilo limeamua kutoa hati hiyo baada ya Flynn, kupitia wakili wake, kukataa kushirikiana na ombi lao la Aprili 28 la kumtaka awasilishe nyaraka hizo.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa hati hiyo kutangazwa na kamati ya ujasusi katika uchunguzi huo. Flynn alifutwa kazi kwa kumdanganya Makamu wa Rais Mike Pence kuhusu mazungumzo yake na balozi wa Urusi mjini Washington. Hayo yanajiri wakati Ikulu ya White House imepuuzilia mbali wito wa kuteuliwa mwendesha mashitaka maalum atakayechunguza madai kuwa timu ya kampeni ya Donald Trump ilishirikiana na Urusi.

USA Richard Burr Senator
Kamati ya ujasusi katika baraza la Seneti inachunguza suala la UrusiPicha: Getty Images/G. Demczuk

Wademocrat waliojawa na hasira wanahoji kuwa kazi ya FBI sasa itatatizwa kabisa baada ya kutimuliwa mkurugenzi wa shirika hilo James Comey na wakadai kuteuliwa mwendesha mashitaka maalum ili kuchunguza suala hilo. Ikulu ya White House ilisema Comey alifutwa kazi kutokana na wasiwasi kuhusiana na namna alivyoshughulikia uchunguzi wa barua pepe za Hillary Clinton. Sarah Huckabee Sanders, ni Msemaji wa Ikulu ya White House

Kwa kweli, nashangaa kuwa hatua hiyo imezusha mgawanyiko kwa sababu warepublican wengi na wademocrat kwa mara nyingi wamekuwa wakitoa wito wa Mkurugenzi Comey kutimuliwa. Kwa kweli sidhani inajalisha anachosema rais, maana lazima tu wademocrat watajitokeza na kumpinga katika kila hatua

Trump aliutetea uamuzi wake huku akipinga madai kuwa ulihusishwa na uchunguzi wa Urusi. Aliwaambia waandishi wa habari kuwa Comey hakuwa akifanya kazi nzuri. Katika barua yake ya kuaga, Comey alisema kuwa kwa muda mrefu aliamini kuwa Rais anaweza kumtimua Mkurugenzi wa FBI kutokana na sababu yoyote au bila sababu yoyote na kwamba hatotumia muda wake mwingi kuzungumzia uamuzi huo na namna ulivyochukuliwa.

Nancy Pelosi
Kiongozi wa upinzani bungeni Nancy PelosiPicha: Getty Images/W. McNamee

Wademocrat waliojawa na hasira, hata hivyo wamesema kazi ya FBI sasa itachafuliwa wakaitaka Wizara ya Sheria kumteuwa mwendesha mashitaka kama wale walioteuliwa na Rais Richard Nixon wakati wa kashifa ya Watergate au wakati wa kipindi cha kabla ya kupigwa kura ya kumfukuza Bill Clinton.

Wanachama kadhaa wa chama cha rais cha Republican, akiwemo kiongozi wa kamati ya ujasusi katika Seneti Richard Burr walijitenga na hatua ya rais. Matamshi ya Trump yalikuja muda mfupi baada ya kumwalika mjumbe mkuu wa Urusi katika Ikulu ya White House, ikiwa nimkutano wake wake wa kwanza wa ana kwa ana wa ngazi ya juu na serikali ya Urusi tangu alipochukua madaraka. Trump aliuelezea mkutano huo na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov kuwa mzuri akisema walizungumzia suala la vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Gakuba Daniel