1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Seneta wa Republican amkosoa vikali Trump

Isaac Gamba
18 Januari 2018

 Seneta wa chama cha Republican nchini Marekani  Jeff Flake amemkosoa vikali rais Donald Trump kwa matamshi yake ya mara kwa mara yanayoonekana kuvishambulia vyombo vya habari .

https://p.dw.com/p/2r3lh
USA Senator Flake Jeff Flake
Picha: picture alliance/AP Images/Senate TV

Akizungumza katika baraza la Seneti la Marekani Jeff Flake amesema  kiongozi yeyote aliyeko madarakani anaposema taarifa ambazo kwa mtizamo wake anaona hakubaliani nazo kuwa ni habari za uwongo basi kiongozi huyo ndiye anapaswa kutiliwa mashaka na siyo vyombo vya habari.

Flake alizidi kumkosoa Trump kwa kutumia baadhi ya maneno yaliyowahi kutumiwa na kiongozi wa zamani wa kiimla wa Urusi Joseph Stalin kuwashambulia wale aliowaona ni maadui zake na kutumia maneno " maadui wa watu "  wakati alipovishambulia vyombo vya habari.

Stalin ambaye alitawala iliyokuwa Jamhuri ya Kisovieti katika kipindi cha kuanzia katikati ya miaka ya 1920  hadi mwaka 1953 ambapo katika kipindi cha utawala wake alituhumiwa kuhusika na vifo vya mamilioni ya watu mara nyingi alitumia maneno hayo kuwashambulia wapinzani wake kisiasa.

Seneta huyo wa Arizona mwenye umri wa miaka 55 ambaye amekuwa mmoja wa wakosoaji wakuu ndani ya chama cha Republican dhidi ya Trump pia alimshambulia kiongozi huyo kutokana na matamshi yake ya kashifa dhidi ya vyombo vya habari kuonekana pia kuuigwa na viongozi wa kiimla kutoka mataifa ya kigeni ikiwa ni pamoja na kuchafua taswira ya vyombo vya habari katika jamii akitolea mfano rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte, Nicolas Maduro waV enezuela  na Bashar Assad wa Syria.

 

Trump ashutumiwa kudhoofisha taasisi za umma

Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/A.P. Bernstein

Aidha seneta huyo alimshutumu rais Trump kwa kujaribu kudhoofisha taasisi za serikali nchini humo akitolea mfano tangu alipo hoji juu ya cheti cha kuzaliwa cha mtangulizi wake Barack Obama  pamoja na kuonekana kuhoji juu ya taarifa zinazoaminiwa na mashirika ya kijasusi ya Marekani kuhusiana na Urusi kudaiwa kuingilia uchaguzi wa mwaka 2016. 

Flake ambaye alitangaza Oktoba mwaka jana kuwa hatawania tena kuchaguliwa  katika uchaguzi utakaofanyika mwaka huu alionya kuwa  pasipo ukweli kusemwa kwa uwazi basi demokrasia nchini humo haiwezi kuendelea kukua.

Hata hivyo msemaji wa Ikulu ya Marekani ya White House Sarah Sanders alionekana kupuuza hotuba hiyo ya seneta Flake akisema seneta huyo hamkosoi  rais Trump kwa vile ni mkandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari bali ni kutokana seneta Flake kutafuta umaarufu.

Hotuba ya Flake inakuja mnamo wakati rais Trump akitarajiwa kutoa tuzo kwa mashirika kadhaa ya vyombo vya habari nchini Marekani  alizozipachika jina " tuzo kwa ajili ya habari za uwongo yaani  (Fake News Awards).

Rais Donald Trump alitoa tangazo hilo wiki iliyopita  kupitia ukurasa wa twitta kuhusiana na mpango wake wa kutoa tuzo hizo kwa vyombo vya habari nchini humo vinavyoongoza kwa rushwa na kutoa taarifa zilizoegemea upande mmoja hatua ambayo seneta Flake ameikosoa pia.

Trump amewahi kusikika akitoa matamshi ya kuvikashifu baadhi ya vyombo vya habari kuwa vinaandika na kutangaza habari za uongo.

Flake ni seneta wa pili na mmoja wa viongozi wanaoheshimika ndani ya chama cha Republican kumkosoa Trump juu ya mahusiano yake na vyombo vya habari baada ya Seneta John Mc Cain  ambaye aliandika makala katika gazeti la Washington Post iliyo na kichwa cha habari " Rais Trump acha kuvishambulia vyombo vya habari"

Mwandishi: Isaac Gamba/dw/afpe

Mhariri: Caro Robi