Schulz aachia wadhifa wa waziri wa mambo ya kigeni
10 Februari 2018Martin Schulz, kiongozi anayeondoka madarakani katika chama cha Social Democratic SPD nchini Ujerumani, hatachukua wadhifa wa waziri wa mambo ya kigeni aliopewa katika serikali mpya ya Ujerumani, akisalim amri kwa mbinyo mkubwa kutoka ndani ya chama chake kabla ya kura muhimu inayotarajiwa kupigwa na chama cha SPD kuhusiana na makubaliano yaliyofikiwa ya kuunda serikali ya mseto na kansela Angela Merkel.
"Natangaza kwamba sitajiunga na serikali ya muungano na wakati huo huo napenda kutoa matumaini yangu kwamba hali hii itamaliza mjadala unaonihusu ndani ya chama cha SPD," Schulz alisema katika taarifa siku ya Ijumaa(09.02.2018). Schulz amekabiliwa na mapambano ndani ya SPD kwa kukubali kwake kuchukua wadhifa huo wa juu wa kidiplomasia baada ya kuahidi kwamba hatakuwa sehemu ya baraza la mawaziri la Merkel.
Tangazo hilo jana Ijumaa lilikuwa ni pigo jingine kwa rais huyo wa zamani wa bunge la Umoja wa Ulaya mwenye umri wa miaka 62, ambaye siku mbili zilizopita alitangaza kuwa anajiuzulu kuwa kiongozi wa chama cha SPD na kumkabidhi madaraka hayo kiongozi wa wabunge wa chama hicho Andrea Nahles.
Hatua hiyo pia inakuja chini ya wiki mbili kabla ya kura itakayopigwa na wanachama 463,723 wa chama cha SPD juu ya iwapo kujiunga ama kutojiunga na serikali ya muungano itakayoongozwa na Merkel.
Aliwasili kama shujaa
Schulz alikuwa amechaguliwa mwaka mmoja uliopita kwa asilimia 100 kukiongoza chama hicho cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto. Aliwasili kama shujaa katika medani ya kisiasa nchini humo Januari mwaka jana, akiahidi kwamba atamwangusha Merkel kama kansela na kukiongoza chama cha SPD katika ushindi.
Baada ya kupanda kwa haraka katika uchunguzi wa maoni ya wapiga kura , uchunguzi wa maoni hayo ulionesha uungwaji mkono wa kile vyombo vya habari vya Ujerumani ilichokieleza kuwa ni treni ya Schulz inayopungua nguvu kwa haraka kabla ya kukiongoza chama hicho kufikia kipigo cha kihistoria mwezi Septemba.
Baada ya hapo alifanya makosa kadhaa makubwa ya kisiasa. Kwanza aliondoa kabisa uwezekano wa kuunda muungano mpya na Merkel na baadaye akakataa kabisa kujiunga na baraza lake la mawaziri.
Miezi michache baadaye alilazimika kufuta uamuzi wake wa kujiunga tena pamoja na Merkel baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya kuunda serikali mwezi Novemba na chama cha walinzi wa mazingira pamoja na kile kinachopendelea biashara cha Free Democrats FDP.
Uungwaji mkono waporomoka
Baada ya kupata asilimia 20.5 tu ya kura katika uchaguzi wa mwezi Septemba , uungwaji mkono wa chama cha SPD ulishuka hadi asilimia 17, kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni ya wapiga kura uliochapishwa wiki hii, ambapo asilimia 72 ya wale walioulizwa wanapinga Schulz kujiunga na serikali mpya.
Kiongozi muhimu wa kundi la SPD limemtaka Sigmar Gabriel kubakia kuwa waziri wa mambo ya kigeni baada ya Schulz kuachana na mipango yake ya kuchukua wadhifa huo.
Sigmar Gabriel anapaswa kubakia kuwa waziri wa mambo ya kigeni. "Bila hivyo sitaelewa kitu", aliandika katika ukurasa wa Twitter Johannes Kahrs, mbunge wa chama cha SPD na msemaji wa kundi la wabunge wa chama hicho bungeni, kundi linalojulikana kama Seeheimer. "Uamuzi wa Martin Schulz unapaswa kutambuliwa na anastahili heshima ya juu kabisa," alisema Andrea Nahles.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Bruce Amani