1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schulz aacha uspika wa EU kuingilia siasa za Ujerumani

24 Novemba 2016

Hatua yake imeibua mjadala wa ni nani atachukua nafasi yake ya Uspika. Nchini Ujerumani inafikiriwa huenda akashindana na Angela Merkel katika kinyang'anyiro cha Ukansela mwakani

https://p.dw.com/p/2TA6V
Deutschland Martin Schulz Statement in Brüssel zu seinem Wechsel in die Bundespolitik
Picha: Reuters/Y. Herman

Rais wa bunge la Umoja wa Ulaya Martin Schulz ametangaza rasmi kuwa ataingilia siasa za Ujerumani mwakani. Inafikiriwa upo uwezekano kuwa huenda atawania kiti cha ukansela. Hali itakayomweka kuwa mpinzani wa Kansela Angela Merkel katika uchaguzi wa mwakani.

Martin Schulz ambaye ni mwanachama wa Social Democratic SPD ametangaza nia hiyo yake leo katika bunge la Umoja wa Ulaya, hivyo kuweka wazi wadhifa wake wa kuwa mkuu wa bunge hilo la Umoja wa Ulaya. Swali likiwa nani atakayechukua nafasi yake, wadadisi wa kisiasa wanasema huenda mrithi wake akatokea kundi la wademokrasia wa kikristo EPP ambao ni wengi katika bunge hilo. Hata hivyo kundi hilo tayari linashikilia nyadhifa za rais wa baraza la Umoja wa Ulaya unaoshikiliwa na Donald Tusk na tume ya urais wa jumuiya hiyo inayoshikiliwa na Jean-Claude Junker.

Akitangaza uamuzi huo Schulz alisema: "Kumekuwa na uvumi kuhusu mustakabali wangu. Sasa nimeshaamua sitawania uspika urais wa bunge la Umoja wa Ulaya kwa muhula wa tatu. Mwaka ujao nitagombea kiti cha bunge la shirikisho la Ujerumani kwa tikiti ya chama change SPD jimbo la North Rhine Vesfalia. Haukuwa uamuzi rahisi, kwani ni heshima kuu kuwa rais wa bunge hili. Ninashukuru kwa nafasi hiyo".

Kansela Angela Merkel akihutubia chama chake CDU
Kansela Angela Merkel akihutubia chama chake CDUPicha: Getty Images/S. Gallup

Nchini Ujerumani, chama cha Schulz SPD, ni chama kidogo katika muungano wa Merkel. Ikiwa Schulz mwenye umri wa miaka 60 atawania ukansela basi atashindana na Merkel kwenye mchujo hasa ikizingatiwa Bi. Angela Merkel alitangaza wiki jana kuwa atawania tena ukansela kwa muhula wa nne hapo mwakani.

Haijabainika ikiwa Schulz ambaye amehudumu kama rais wa bunge la Umoja wa Ulaya tangu mwaka 2012, ndiye atakayekuwa mgombea mkuu wa chama chake SPD. Kwa sasa Naibu Kansela Sigmar Gabriel ndiye anayeongoza katika chama hicho cha SPD, lakini anakabiliwa na umaarufu wa chini kulingana na matokeo ya kura za maoni.

Huku chama cha SPD kikitarajiwa kumtangaza mgombea wake rasmi mwisho wa mwezi Januari, hadi sasa hakuna uamuzi ambao umefikiwa wa ni nani atakayekuwa mshindani wa Merkel kwenye kinyang'anyiro cha Ukansela.

Aidha inafikiriwa huenda Schulz akawa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, kuchukua nafasi ya Frank Walter Steinmeier ambaye anatarajiwa kuacha wadhifa wake mapema mwaka ujao kwani ameshateuliwa kuwania urais.

Mwandishi: John Juma/RTRE/FPE

Mhariri:Josephat Charo