1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz ataka Ulaya yenye mageuzi na mtazamo wa kidunia

Daniel Gakuba
9 Mei 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amelihutubia Bunge la Ulaya mjini Strasbourg nchini Ufaransa, ambamo amegusia masuala kadhaa yanayopaswa kujumuishwa katika sera ya Ulaya, kwa ajili ya mustakabali wenye amani na ustawi.

https://p.dw.com/p/4R59N
Olaf Scholz und Roberta Metsola, Präsidentin Europäisches Parlament
Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz (kushoto), na Spika wa Bunge la Ulaya Roberta Metsola bungeni mjini StrasbourgPicha: Bernd Riegert/DW

Katika hotuba hiyo aliyoitoa mjini Strabourg, Kansela Olaf Scholz ametoa wito wa kuupanua Umoja wa Ulaya na kuufanyia mageuzi, ili uwe na fikra na vitendo vinavyoakisi nafasi yake katika jumuiya ya kimataifa.

Amesema nchi wanachama wa umoja huo hazina budi kuwianisha sera zao za mambo ya nje na kodi, na kutimiza ahadi ya kuyapa uanachama mataifa ya magharibi mwa ukanda wa Balkan.

Soma zaidi: Kansela Scholz azungumza na Rais Ruto

Kiongozi huyo wa Ujerumani ameushauri Umoja wa Ulaya kujadili mipango ya biashara huria na nchi za mabara tofauti, akizitaja Argentina, Brazil, Paraguay, India, Indonesia, Australi na Kenya miongoni mwa nyingine.

Papst Franziskus Europäisches Parlament Straßburg
Bunge la Ulaya mjini Strasbourg, Ufaransa huwa linatoa jukwaa kwa viongozi mashuhuri kutangaza sera zao.Picha: Patrick Seeger/AP Images/picture alliance

Ulaya yapaswa kuachana na fikra za kale

Ili kufanikisha ushirika huo, Kansela Scholz amesema Ulaya inalazimika kuzipatia jibu kero zilizoachwa na utawala wa kikoloni katika nchi za Afrika na Asia, na kufanya kazi na nchi hizo kama washirika.

''Kuzikabili changamoto hizo, inatubidi kuzidisha ushirikiano na maeneo mengine ya dunia, hususan Asia na Afrika ambazo hivi karibuni nilizitembelea,'' amesema Scholz na kuongeza  kuwa ''tunapaswa kufanya kazi na nchi hizo kama washirika, na kuwa Umoja wa Ulaya wenye mtazamo wa kidunia.''

Soma zaidi: Macron: Ulaya haipaswi kujitenga na China

Kansela huyo ameongeza kuwa Ulaya haina bundi kuachana na mitazamo ya karne zilizopita, na kuhakikisha usalama wa chakula, kupiga vita umasikini na kuyalinda mazingira.

Akionekana kutofautiana na mtazamo wa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambaye hivi karibuni alipigia debe Ulaya imara na iliyo huru, isiyoegemea upande wa mataifa mengine makubwa kama Marekani na China, Kansela Olaf Scholz amesema ''wale wanaong'ang'ania ndoto ya Ulaya kama taifa kubwa wamenaswa katika zama za kale.''

EU Parlament | Sakharov-Preis für die Ukraine
Vita vya Ukraine ni mojawapo ya masuala yanayolishughulisha sana Bunge la Ulaya kwa wakati huuPicha: Frederick Florin/AFP

Gwaride la jeshi la Putin ''zisitutishe''

Kuhusiana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, Kansela wa Ujerumani ametaka Ulaya iendelee kusimama bega kwa bega na Ukraine, katika juhudi zake za kujilinda, na za ukarabati siku za baadaye.

Aidha, amegusia sherehe za kijeshi zilizokuwa zikiendelea mjini mjini Moscow wakati akiitoa hotuba yake,  ambapo Urusi inaadhimisha ushindi dhidi ya Ujerumani iliyotawaliwa na Wanazi, akisema gwaride na maonyesho ya kijeshi vinavofanywa na Rais Vladimir Putin haviwezi kuitisha Ulaya.

Soma zaidi: Von der Leyen awarai viongozi wa Ulaya kushikamana kuikabili China

Sera kuelekea China na kuimarika kwake kiuchumi na kiushawishi ni suala jingine aliloligusia Kansela Olaf Scholz katika hotuba yake mbele ya bunge la Ulaya.

Kuhusu ili, ameunga mkono mtazamo wa rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, kuwa inachopaswa kukifanya Ulaya sio kukatisha mahusiano na China, bali kuhakikisha kuwa ushirikiano huo sio kitisho kwa usalama wa Ulaya na maslahi yake.

Vyanzo: dpae, afpe