1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schalke na FC Kolon zapata pointi mara ya kwanza msimu huu

Sekione Kitojo
19 Oktoba 2020

Bayern Munich bado yawasha moto katika  Bundesliga , wakati Schalke na FC Kolon zapata pointi kwa mara ya kwanza  msimu huu.

https://p.dw.com/p/3k96e
Deutschland Bundesliga 1. FC Köln gegen Eintracht Frankfurt Tor Köln
Wachezaji wa FC Kolon wakisherehekea bao la kusawazisha dhidi ya Eintracht FrankfurtPicha: Marcel Kusch/AFP/Getty Images

Katika  Bundesliga, Schalke imesogea kidogo  kutoka  katika  nafasi ya  mwisho katika  msimamo wa ligi  ya Ujerumani  baada  ya  kutoka sare ya bao 1-1 jana  dhidi  ya  Union Berlin lakini wameendeleza rekodi ya  klabu hiyo  kutoshinda  mchezo  katika  michezo 20  hadi sasa. Goli la kichwa la  Goncalo Paciencia liliwapa schalke pointi moja ya kwanza msimu huu wakati kocha  mpya  Manuel Baum akisimamia  mchezo wake wa kwanza wa timu  yake akiwa nyumbani. Wamesogea juu  hadi  nafasi ya 17, na  ni  Mainz 05  tu ambayo  haina  pointi  hadi  sasa  imebakia  katika  nafasi ya mwisho, wakati  FC Kolon wamesogea  katika  nafasi ya  16 baada ya  kutoka  sare na  Eintracht Frankfurt jana  Jumapili. Huyu hapa kocha wa Schalke 04 Manuel Baum.

Deutschland Bundesliga 1. FC Köln gegen Eintracht Frankfurt
Elvis Rexhbecaj wa FC Koln akidhibiti mpira wakati wa pambano kati ya FC na EintrachtPicha: Mika Volkmann/Getty Images

"Kama mtu akiangalia mchezo huu, nafikiri hatuwezi kusema kwamba tumefurahishwa na mchezo wetu. Tumepiga hatua katika mchezo wetu , lakini mtu anatambua vipi mchezo huo umewagusa wachezaji. Na unapofungwa  goli, lazima niseme wazi, kwamba nimefurahishwa, na  jinsi wachezaji  walivyopambana baada  ya  bao hilo na hatimaye kurejesha bao."

FC Kolon nao walipata  pointi yao ya kwanza  msimu huu, baada  ya kutoka  sare  ya  bao 1-1 dhidi  ya  Eintracht Frankfurt , ikiwa  ni mwanzo mzuri kwa  timu  hiyo  ambayo  nayo  imekuwa  ikipata matokeo  mabaya  tangu mwishoni mwa  msimu  uliopita. Mchezaji wa FC Kolon Sebastian Bornauw alikuwa  na  haya  ya  kusema.

Bundesliga Arminia Bielefeld vs. FC Bayern München
Kingsley Coman wa Bayern akipambana na Nathan De Medina wa BielefeldPicha: Sascha Steinbach/Getty Images

"Nafikiri, kwamba  ni pointi muhimu kwetu. Tulikuwa na matumaini ya pointi tatu, lakini  pointi moja ni bora  kwa mchezo huu. Nafikiri , dakika  20  za  mwanzo  katika  kipindi cha  pili tuliweza  kuonesha mchezo mzuri  zaidi  katika  msimu  huu. Ni lazima  katika  mchezo ujao tujaribu, kufanya  kama  hivi kuanzia  mwanzo."

Mabingwa watetezi Bayern Munich waliikandamiza  Arminia  Bielefeld kwa  mabao 4-1 siku  ya  Jumamosi baada  ya  Leipzig  kushinda kwa  mabao 2-0 nyumbani  kwa  Augsburg.  Borussia  Dortmund ilipata ushindi  wa  kibarua pale ilipoishinda timu inayoipa  taabu sana mara kadhaa TSG Hoffenheim kwa  bao 1-0  katika  mchezo ambao timu zote zilionesha  uwezo mkubwa. Nahodha  wa Borussia Dortmund Marco Reus naye alikuwa na haya ya kusema.

Fußball 1. Bundesliga | Borussia Dortmund | Marco Reus
Nahodha wa Borussia Dortmund, Marco Reus Picha: picture-alliance/SvenSimon/E. Kremser

"Hoffenheim imeishinda Bayern  hapa wiki mbili zilizopita. Hususan jinsi walivyowashinda ilikuwa inavutia sana na  leo  ilikuwa tunatarajia  mchezo mgumu pia. Hatujacheza mchezo mzuri sana,  hii ni  wazi. Lakini pia  ilikuwa ni vigumu , wakati wachezaji wa  timu za taifa  walirejea tu siku ya Alhamis au Ijumaa. hatukuweza kufanya mazowezi ya pamoja kabisa, kwa hiyo huo ulikuwa ushindi wa kibarua. Lakini kesho hakutakuwa na mtu atakayeuliza hilo."

Timu iliyopanda daraja msimu huu VFB Stuttgart imerejea  kwa kishindo  katika  ligi ya  Bundesliga  baada  ya  kuichapa  Hertha Berlin  kwa  mabao 2-0 ugenini.