Schalke na Dortmund kuumiza nyasi
8 Machi 2013Schalke wameshinda tu mmoja kati ya mechi zao tano za mwisho za Bundesliga dhidi ya Dortmund, lakini wageni hao ambao wako katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi, watataka kulipiza kisasi kichapo cha magoli mawili kwa moja katika uga wa Uwanja wa Dortmund Signal Iduna Park mwezi Oktoba. Nahodha Sebastian Kehl na beki wa katikati Sven Bender wanakabiliwa na mtihani mgumu wa kuwa katika hali shwari baada ya kucheza katika mchuano wao walioshinda Shakhtar magoli matatu kwa sifuri. Schalke ambao watapambana na Galatasaray katika ligi ya mabingwa Jumanne ijayo, katika uga wa nyumbani wa Gelsenkirchen, baada ya sare ya magoli mawili kwa mawili mjini Istanbul, wamerejea hali yao nzuri baada ya kupata ushindi mara mbili mfululizo na wako katika nafasi ya sita kwenye ligi. Kiungo wa Schalke Jermaine Jones hatacheza mchuano huo, wakati Robert Lewandoswki ambaye amefunga magoli sita katika kila mchuano kati ya sita za mwisho katika Bundesliga.
Kwingineko, Mshambuliaji wa Bayern Munich Mario MANDZUKIC amesema kwamba miamba hao wa Bundesliga wanalenga kuwabwaga Fortuna Düsseldorf katika Bundesliga leo Jumamosi kama matayarisho ya mchuano wa wiki ijayo wa Ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya Arsenal.
Huku wakiwa kileleni mwa ligi na pengo la pointi 17, na zikiwa zimesalia mechi kumi msimu kukamilika, Bayern wanatoroka na taji la msimu huu la Bundesliga, lakini wanalenga pia kusajili ushindi wa kumi mfululizo nyumbani dhidi ya Fortnuna, ambao wako katika nafasi ya 12. Bayern wanalenga kuimarisha uongozi wao kabla ya kukutana na Arsenal katika mechi ya mkondo wa pili wa kufuzu katika robo fainali dhidi ya Arsenal Jumatano wiki ijayo.
Ushindi wa mwisho wa Fortnuna dhidi ya Bayern katika Bundesliga ulikuwa Aprili mwaka wa 1991 na Munich wameshinda mechi zao zote tatu za mwisho dhidi yao bila kufungwa goli hata moja.
Wachezaji nyota wa Bayern Arjen Robben na Bastian Schweinsteiger wamefanya mazoezi wiki hii baada ya kupona majeraha, wakati Mario Gomez, hasimu mkubwa wa Mandzukic akikatiza mazoezi kutokana na jeraha dogo la mguu.
Klabu inayoshika mkia Greuther Fürth inawaalika Hoffenheim, ambao wako juu yao pointi moja pekee. Mechi nyingine za leo Jumamosi ni kati ya Freiburg v VfL Wolfsburg, Mainz 05 v Bayer Leverkusen, na Borussia M'gladbach v Werder Bremen. Jumapili, (09.03.2013) Hanover 96 v Eintracht Frankfurt, VfB Stuttgart v Hamburg.
Mkufunzi wa Manchester City Roberto Mancini amepuuzilia mbali uvumi unaomusisha mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney kujiunga na klabu hiyo. Hatma ya Rooney katika klabu ya United imekuwa ikiangaziwa sana katika siku za karibuni baada ya kubakia nje kama mchezaji wa akiba katika mchuano wao wa Ligi ya mabingwa walioshindwa na Real Madrid magoli mawili kwa moja. Mkufunzi wa United Sir Alex Ferguson hata hivyo amesisitiza kuwa Rooney haendi kokote na kwamba atasalia katika klabu hiyo msimu ujao, akisema hawana tofauti zozote baina yao. City walimtaka Rooney mwenye umri wa miaka 27, wakati alionekana kugura Old Trafford mnamo mwaka wa 2010. lakini Mancini amekaata uwezekano wa kumleta tena katika klabu hiyo. Mancini anatarajiwa kuiimarisha safu yake ya mashambulizi kufuatia kuondoka kwa Mario Baloteli aliyejiunga na AC Milan mwezi Januari.
Carlos Tevez atakuwa na mwaka mmoja pekee uliosalia kwenye mkataba wake na pia kuna uvumi kwamba mshambuliaji wa zamani wa Wolfsburg Edin Dzeko huenda akarudi tena katika Bundesliga kujiunga na Borussia Dortmund. Mancini anakiri kuwa kubanduliwa nje Manchester United katika Ligi ya Mabingwa kutaathiri juhudi za City kuwania taji la ligi.
United wanawaalika Chelsea katika mchuano wa robo fainali wa kombe la FA kesho Jumapili na Fergie amesema kwamba Rooney atashiriki mchezo huo. Chelsea wameshindwa goli moja kwa sifuri na klabu ya Steua Bucharest katika mchuano wao wa kufuzu awamu ya 16 za mwisho katika Europa League.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman