1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudia yamualika Bashir kukutana na Trump

Daniel Gakuba
17 Mei 2017

Saudi Arabia imemwalika Rais Omar al-Bashiri wa Sudan ambaye anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) katika mkutano wa kilele wa viongozi wa Kiarabu na Kiislamu na Rais Donald Trump wa Marekani.

https://p.dw.com/p/2d690
Kigali Omar Bashir AU Gipfel
Picha: picture-alliance/dpa/P.Siwei

Afisa aliyezungumza na shirika la habari la AFP hakusema iwapo Rais al-Bashir atakuwepo katika mkutano wa mwisho wa ngazi ya juu kabisa siku ya Jumapili.

Kuanzia Jumamosi, Rais Trump anatarajiwa kufanya ziara nchini Saudi Arabia ambako kuna sehemu takatifu kabisa za kiislamu, hiyo ikiwa ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu alipochukua hatamu za uongozi mwezi Januari.

Rais Bashir ameweza kukwepa kukamatwa tangu alipowekewa waranti na Mahakama ya Kimataifa mwaka 2009, kwa tuhuma za mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu vilivyofanywa katika jimbo la Darfur, ambako watu wasiopungua 300,000 wamepoteza maisha.