Saudi Arabia yatangaza muungano wa kijeshi wa kiislamu
15 Desemba 2015Tangazo hilo limechapishwa na shirika la habari la Saudi Arabia na kuongeza muungano huo utaongozwa na nchi hiyo na umeanzishwa kwa sababu ugaidi unapaswa kukabiliwa kwa kutumia kila njia na ushirikiano huo utakuwa njia mwafaka utakao uangamiza.
Taarifa hiyo inasema Uislamu unapinga ufisadi na maangamizi na ugaidi unakiuka hadhi na haki za binadamu hasa haki ya kuishi na kuwa salama. Miongoni mwa nchi zitakazoshiriki katika muungano huo ni Pakistan, Uturuki, Misri, Libya na Yemen. Mali, Chad, Somalia na Nigeria pia ni wanachama wa muungano huo mpya wa kupambana dhidi ya ugaidi.
Hasimu wa muda mrefu wa Saudi Arabia, Iran haijajumuishwa katika muungano huo. Saudi Arabia na Iran zimekuwa zinayaunga mkono makundi tofauti katika mizozo ya Yemen na Syria. Oman pia haijashirikishwa katika muungano huo wa kijeshi.
Asasi za kimataifa zitashirikishwa
Katika mkutano na wanahabari, mwana wa mfalme wa Saudi Arabia ambaye ni waziri wa ulinzi Mohmmed bin Salman amesema muungano huo wa kijeshi wa nchi za kiislamu utaunda mfumo wa kushirikiana na nchi nyingine na asasi za kimataifa katika kuunga mkono juhudi za kupambana na ugaidi na kwamba hawajikita tu katika kulikabili kundi la wanamgambo wenye itikadi kali wa dola la kiislamu IS. Mwanamfalme huyo amesema kitisho cha ugaidi ni kikubwa
''Leo kuna mataifa kadhaa yanayokumbwa na ugaidi, kwa mfano Dola la Kiislamu nchini Syria na Iraq, ugaidi Sinai, ugaidi Yemen, ugaidi Libya ugaidi Mali, ugaidi Nigeria, ugaidi Pakistan, ugaidi Afghanistan na hili linahitaji juhudi thabiti ili kupambana nao'' Amesema mwanamfalme Salman, na kuongeza kuwa Bila shaka kutakuwa na ushirikiano katika juhudi hizo.
Kama Iran, Oman pia yatengwa
Mataifa wanachama wa muungano huo ni pamoja na taifa dogo la Maldives na taifa la kisiwani cha Bahrain katika Ghuba ya wajemi ya kiarabu, ambayo pia ni makao makuu ya jeshi la majini la Marekani. Mataifa mengine ya ghuba ambayo yameshirikishwa katika muungano huo ni Kuwait,Qatar na falme ya milki za kiarabu. Oman ambayo ni jirani ya Saudi Arabia haipo katika muungano huo. Siku za hivi karibuni Oman imekua ikishikilia msimamo wa wastani kama mpatanishi katika mzozo wa mashariki ya kati.
Wanachama wote wa muungano huo pia ni sehemu ya Shirika kubwa ya Ushirikiano wa Kiislamu, ambayo makao yake makuu yako nchini Saudi Arabia. Uturuki ndio mwanachama wa pekee wa shirika la kujihami la Nato kujiunga na Muungano huo.
Mwandishi: Ambia Hirsi/APE/
Mhariri: Daniel Gakuba