Saudi Arabia yataka Iran ijibiwe kwa nguvu zote
30 Mei 2019Marekani na baadhi ya maafisa wa mataifa ya Kiarabu wanadai mashambulizi hayo yalifanywa na Iran.
Waziri al-Assaf ametoa matamshi hayo katika mkutano wa maandalizi wa mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa 57 yanayounda Jumuiya na mataifa ya Kiarabu OIC kuelekea mikutano mitatu ya kilele itakayofanyika kwenye mji mtakatifu wa Mecca.
Saudi Arabia inataka kutumia mkusanyiko huo wa mjini Mecca kutuma ujumbe thabiti na wa wazi kwa Iran ambayo pia ni mwanachama wa OIC.
Kwenye hotuba ya ufunguzi al-Assaf amesema mashambulizi dhidi ya meli za mafuta katika pwani ya Umoja wa Falme za Kiarabu na yale yaliyofanywa na ndege zisizokuwa na rubani na waasi wa Houthi wa Yemen wanaoungwa mkono na Iran kwenye mabomba ya mafuta nchini Saudi Arabia, yanatishia uchumi wa dunia na kuhatarisha usalama wa kikanda na kimataifa.
Alisema, "Ufalme wa Saudi Arabia unasisitiza kuwa vitendo hivi vya uwoga vinatishia uchumi wa dunia na vinauweka hatarini, usalama wa kikanda na kimataifa na lazima vikabiliwe kwa nguvu na uthabiti."
Saudi Arabia, imeitisha mikutano hiyo kujadiliana kuhusu kuongezeka kwa wasiwasi na hasimu wake muhimu Iran. Iran iliwakilishwa na afisa mmoja kwenye ufunguzi wa mkutano huo, lakini waziri wa mambo ya nje, Mohammad Javad Zarif hakuhudhuria.
Mkutano wa kwanza wa kilele kati ya hiyo mitatu utaanza kwa kikao cha viongozi wakuu wa mataifa sita yanayounda Baraza la ushirikiano wa mataifa ya Ghuba Alhamisi jioni.
Waziri mkuu wa Qatar, Sheikh Abdullah bin Nasser Al Thani anatarajiwa kuhudhuria na kuifanya ziara yake nchini Saudi Arabia kuwa ya ngazi ya juu zaidi kufanywa na afisa wa Qatar tangu mwaka 2017 wakati taifa hilo la Kifalme na mengine matatu ya Kiarabu yalipokata mahusiano ya kidiplomasia na Qatar, kuhusiana na sera zake za kigeni.
Mkutano huo utafuatiwa na mkutano wa kilele wa dharura wa mataifa 22 ya Jumuiya ya nchi za Kiarabu ukiondoa Syria ambayo uanachama wake umesimamishwa. Mkutano wa tatu na wa mwisho wa kilele utakaofanyika kesho Ijumaa unatarajiwa kuangazia kwa mapana hadhi ya Palestina na uhuru wa taifa hilo.
Miongoni mwa wanaohudhuria ni rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, waziri mkuu wa Lebanon, Saad Hariri, rais wa Misri, Abdel-Fattah el-Sissi na Amiri wa Kuwait, Sheikh Sabah Al Sabah.