Saudi Arabia yakata mahusiano na Canada
8 Agosti 2018Jumatatu wiki hii Saudi Arabia ilimpa saa 24 balozi wa Canada nchini humo Dennis Horak kuondoka nchini humo na kutangaza ni mtu asiyetakiwa kabisa katika taifa hilo huku pia ikitangaza kuwa mahusiano yote mapya ya kibiashara kati yake na Canada yatasitishwa.
Hatua hiyo inafuatia ujumbe kupitia ukurasa wa twitter ulioandikwa wiki iliyopita na waziri wa mambo ya nje wa Canada Chrystia Freeland akisema Canada ina wasiwasi mkubwa na kuendelea kutiwa mbaroni wanaharakati wa haki za binadamu na za wanawake nchini Saudi Arabia akiwemo Samar Badawi ambapo Freeland alitoa mwito kwa serikali ya Saudi Arabia kuwaachia huru haraka.
Saudi Arabia imekosoa ujumbe huo kupitia ukurasa wa twitter ikisema unaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na kuwa unakiuka sheria za taifa hilo la Kifalme na pia mfumo wake wa kimahakama.
Aidha Saudi Arabia imesema itazuia maelfu ya wanafunzi wa nchi hiyo kwenda kusoma Canada huku shirika la ndege la nchi hiyo likitangaza kusitisha safari zake kwenda Canada kuanzia August 13.
Mataifa kadhaa ya kiarabu katika ukanda huo yameonesha kuunga mkono hatua ya Saudi Arabia dhidi ya Canada huku Anwar Gargash waziri wa mambo ya nje katika Umoja wa Falme za Kiarabu akisema wataendelea kuiunga mkono Saudi Arabia katika kulinda mamlaka yake.
Kwa upande wake Mohammad bin Abdullah al-Zulfi mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mjumbe wazamani wa baraza la ushauri nchini humo alisema anaunga mkono hatua iliyochukuliwa na mwana wa mfalme Mohammad bin Salman pamoja na serikali yake dhidi ya Canada. Ameieleza DW kuwa Saudi Arabia ni taifa kubwa na haihitaji Canada, Ujerumani au Marekani.
Marekami yasema hilo ni suala lakidiplomasia
Hayo yanajiri huku Marekani ikisema suala kati ya Saudi Arabia na Canada ni la kidiplomasia na litapaswa kutafutiwa ufumbuzi na nchi zote mbili.
Kwa upande wake Umoja wa Ulaya umesema wanahitaji maelezo kuhusiana na hatua ya kukamatwa wanaharakati wa haki za wanawake nchini Saudi Arabia.
Maja Kocijancic msemaji wa Umoja wa Ulaya amesema wamekuwa wakiitaji ufafanuzi tangu Mei mwaka huu kutoka Saudi Arabia kuhusiana na hatua ya nchi hiyo kuwatia mbaroni wanaharakati kadhaa.
Amesema Umoja wa Ulaya unataka kufahamu vema kuhusiana na tuhuma dhidi ya wanaharakati na kuhakikisha wanatendewa haki katika shauri lao.
Hii si mara ya kwanza Saudi Arabia kuingia katika mzozo wakidplomasia kuhusiana na suala la mwanaharakati Badawi kwani mwaka 2015 iliwahi kumuita balozi wake nchini Sweden baada ya waziri wa mambo ya nje wa Sweden kukosoa uamuzi wa mahakama kuhusiana na kesi ya mwanahakati huyo hatua iliyofuatiwa na kusimamisha viza za kazi nchini humo kwa raia wa Sweden.
Mwandishi: Isaac Gamba/DW/APE
Mhariri: Iddi Ssessanga